Trending News>>

Cuba na Zanzibar kushirikiana kuimarisha Sekta ya Utalii

Jamuhuri ya Watu wa Cuba inakusudia kuandaa Mpango maalum utakaoziwezesha Wizara  zinazosimamia Sekta ya Utalii kati ya Nchi hiyo na Zanzibar  kushirikiana katika kuimarisha huduma za  Utalii na masuala yaUtamaduni ili kustawisha urafiki wa pande hizo.
Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandes alitoa kauli hiyo wakati wa Mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi yaliyofanyika kwenye Makaazi yake Mjini Dar es salaam.
Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandes Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Nyumbani kwake Jijijini Dar es salaam kwa ajili ya mazungumzo ya urafiki wa Nchi zao.
Profesa Lucas Domingo Hernandes alisema mpango huo utahusisha kuangalia fursa za kuanzishwa kwa mikataba ya Ushirikiano itakayolenga kuheshimu na kuendeleza uhusiano ulioanzishwa na Waasisi wa Mataifa hayo Marehemu Fidel Castro wa Cuba na Mwalimu Julius  K. Nyerere wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema Zanzibar na Cuba ni Visiwa vyenye mazingira   yanavyofanana  hasaTamaduni zake kiasi kwamba juhudi za pamoja zinastahiki kuchukuliwa ili kuona Uchumi, Maendeleo pamoja na maisha ya Wananchi wa pande hizo mbili yanaendelea kustawi kila wakati.
Profesa Lucas alisema zipo Sekta zilizoleta ufanisi  na kuifaidisha Jamii kwa kiwango kikubwa tokea kuanzishwa kwa ushirikiano  wa pande hizo mbili akitolea mfano ile ya Afya ambayo mafanikio yake yameshuhudiwa na Wananchi walio wengi.
Balozi Lucas Domingo Kushoto akisisitiza azma ya Cuba kuendelea kuunga mkono Kitaaluma Jitihada za Serikali ya Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika mustawisha miradi ya Maendeleo.
Balozi wa Cuba Nchini Tanzania alimuhakikishia  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba  Cuba itaendelea kuunga Mkono jitihada zinazochukuliwa na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika kusaidia Taaluma kwenye sekta tofauti za Maendeleo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mpango wa Serikali ya Cuba kupitia Wizara ya Afya Zanzibar wa kusomesha Madaktari Wazalendo umeleta faraja na kuimarisha uhusiano wa Nchini Mbili hizo.
Balozi Seif alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Sekta ya Afya tokea kumalizika kwa mafunzo ya awamu ya kwanza ya kundi kubwa la Madaktari Wazalendo ambapo huduma za matibabu zimezidi kuimarika katika Hospitali na vituo mbali mbali vya Afya Visiwani Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi Lukas kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha ulinzi wa Wahadhiri wa Chuo cha Madaktari  pamoja na Madaktari wanaotoa huduma za Matibabu na Taaluma Zanzibar licha ya ishara za vitisho iliyowahi kujitokeza dhidi ya wataalamu na Madaktari hao.
Balozi Lucas Kushoto akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif zawadi inayovutia ya Ramani ya Mji wa Havana itakayomsaidia kwa kumbu kumbu zake za baadae.

Balozi Lucas Domingo Kulia akimshindikiza Mgeni wake Balozi Seif mara baada ya kumaliza mazungumzo yao ya ushirikiano wa uhusiano wa Nchi zao mbili {Zanzibar na Cuba }.

No comments:

Powered by Blogger.