AFYA YAMWAGA AJIRA 3,000 KWA MADAKTARI, WAUGUZI
SERIKALI
imesema wiki ijayo itatoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya
vikiwemo vya madaktari na wauguzi pamoja na maofisa hesabu 535 kwa ajili
ya vituo vya afya vya kata ili washughulike na ukusanyaji wa mapato
kwenye vituo vya afya na zahanati.
Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Dk Laurean Ndumbaro alisema hayo jana mjini hapa wakati wa kufungua
kikao kazi cha waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu maadili na
uwajibikaji mahali pa kazi. Dk Ndumbaro alisema vibali hivyo vitatolewa
wiki ijayo kwa madaktari, wauguzi na maofisa wa mahesabu 535.
“Maofisa
hesabu 535 wataajiriwa kwa ajili ya vituo vya afya vya kata na tumeamua
kuwa na maofisa wa hesabu katika vituo vyote vya afya, waganga wakuu wa
wilaya watangaze nafasi na waanze kushughulikia ukusanyaji mapato
kwenye vituo vya afya na zahanati zilizopo ndani ya kata,” alisema Dk
Ndumbaro na kuwataka viongozi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria kanuni
na taratibu ili kujenga utumishi wa umma wenye uadilifu.
“Wanaoharibu
wasihamishwe na kupelekwa maeneo mengine ukifanya hivyo utakuwa
unaharibu utumishi wa umma, ufumbuzi ni kuchukua hatua palepale alipo
usimuhamishe kwenye kituo,” alisisitiza. Pia alitaka kujengwa kwa
utamaduni wa kuwapongeza watumishi wa umma wanaofanya vizuri kwenye
maeneo yao ya kazi.
Chanzo-Habarileo
No comments:
Post a Comment