Wananchi wa Tarime Wavamia Mgodi wa North Mara
Siku
chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kukabidhiwa ripoti ya pili ya
kuchunguza mchanga wa dhahabu wa Kampuni ya Madini ya Acacia, wananchi
wa Tarime wamevamia mgodi wa North Mara kwa siku mbili mfululizo.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni mwendelezo wa kupinga uonevu unaofanywa na wawekezaji hao kupitia Kampuni ya Acacia.
Taarifa kutoka wilayani Tarime zinadai kuwa wananchi hao walivamia mgodi huo juzi saa 2.00 usiku na jana asubuhi.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, wananchi hao walikwenda hadi kwenye mtambo wa
kufua dhahabu na kufanya uharibifu huo kabla ya kudhibitiwa na jeshi
la polisi.
Hata
hivyo shuhuda huyo ambaye hakutaka kutaja jina , alisema vurugu hizo
zimetokana na uongozi wa Kampuni ya Acacia kushindwa kuwalipa fidia
wananchi waliokuwa na maeneo yao tangu awali.
Alisema
wakati madini yalipogundulika, wananchi walioondolewa walitathiminiwa
mali zao yakiwamo mashamba, nyumba na kuahidiwa kulipwa fidia akini
hadi sasa hawajalipwa stahiki zao.
Alisema
kwa siku mbili mfululizo wanachi wenye madai yao walifika katika ofisi
za kampuni na kuona baadhi ya majina ya wanaotakiwa kulipwa fidia
yakiwa yamebandikwa katika ubao wa matangazo lakini majina ya wengine
yakiwa hayajabandikwa.
“Wale
ambao hawakuona majina yao walichukuana na kuvamia mtambo wa kufua
madini na kuondoka na mawe ambayo tunahisi mengine yana dhahabu.
“Lakini polisi walifika na kuwatawanya na mabomu ya machozi,’’ kilisema chanzo cha habari hiyo.
Alipotafutwa
kuzungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga,
alisema alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya
ingawa aliahidi kuzungumza na waandishi wa habari leo.
“Nimesema
hivi, siwezi kuzungumza lolote, sina cha kuzungumza na siwezi
kuzungumza na mwandishi hadi hapo tutakapokaa kikao kesho (leo) ndiyo
nitasema,’’alisema Luoga.
Alipotafutwa
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) kujua kama hatua ya
wananchi hao inatokana na kauli yake aliyoitoa bungeni hivi karibuni
kuwa atawaongoza wananchi kuwaondoa Acacia kwa kuwa wamekuwa
wakiwaibia kama ilivyoelezwa kwenye ripoti ya Tume ya Rais Magufuli,
alisema kwa sasa yupo Dodoma kwa ajili ya vikao vya Bunge .
Alisema anachojua ni kuwa wananchi hao wamekuwa wakidai malipo yao kwa muda mrefu.
“Wananchi
wamekuwa na malalamiko wakidai malipo yao na tayari mgodi umeshaleta
madhara mengi, hilo naweza kusema lakini mengine zaidi ya hayo siwezi
kuyajua,’’ alisema Heche.