Stars yawasili salama Afrika kusini....
Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wa wasili salama Afrika kusini
Kikosi cha wachezaji 22 wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kimesafiri na
kufika salama nchini Afrika Kusini kikitokea Dar es Salaam, Tanzania.
Timu hiyo iliyoondoka jana Alhamisi Juni 22, 2017 kwenda Afrika Kusini
kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda, itakuwa huko kwa ajili ya
michuano ya kuwania Kombe la Castle Cosafa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti, itaanza kampeni za
kucheza hatua ya Robo fainali kwa kucheza na Malawi Jumapili, Juni 25,
mwaka huu katika michuano hiyo iliyoandaliwa na Baraza la Mpira wa Miguu
la nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa).
Tanzania si mwanachama wa Cosafa, lakini imealikwa katika mashindano
hayo na imepangwa kundi A na timu za Mauritius, Malawi na Angola wakati
Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Kinara wa kila
kundi atakwenda moja kwa moja hatua ya robo fainali.
Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na
Swaziland tayari zimepangwa hatua ya robo fainali hivyo zinasubiri
vinara wawili kutoka makundi ya A na B kuungana nazo kucheza robo
fainali.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Shabani Mayanga, amesema kwamba
anaichukulia michuano hiyo kwa umakini na uzito mkubwa kwa wachezaji
kuzidi kupata uzoefu wa mechi nyingi za kimataifa kwa mwaka.
Kadhalika, kiufundi Mayanga anachukulia michuano hiyo kama sehemu ya
maandalizi makubwa ya mchezo dhidi ya Rwanda wa kuwania kucheza nafasi
ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji
wanaocheza ligi za ndani – CHAN.
Mchezo huo wa kwanza utafanyika Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Kikosi cha Taifa Stars kilichopo Afrika Kusini kinaundwa na makipa Aishi
Salum Manula (Azam FC), Benno David Kakolanya (Young Africans SC) na
Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC).
Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Salum Kapombe (Azam FC) na
Hassan Hamis Ramadhan ‘Kessy’ (Young Africans SC) wakati upande wa
kushoto wapo Gadiel Michael (Azam FC) na Hamim Abdulkarim (Toto Africans
FC).
Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa
Sugar), Abdi Hassan Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons)
wakati viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao Mkami (Azam FC) na Salmin
Hoza wa Mbao FC.
Kadhalika wako viungo wa kushambulia ambao ni Mzamiru Yassin Selembe
(Simba), Simon Happygod Msuva (Young Africans SC), Raphael Daudi (Mbeya
City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba SC).
Katika safu ya ushambuliaji wamo Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC
Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili
Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).
No comments:
Post a Comment