Trending News>>

ELIMU::Walimu kula bingo kozi ya Kimataifa .




ZAIDI ya walimu wakuu na maofisa elimu 25 kutoka wilayani Ngorongoro, Halmashauri ya Jiji la Arusha wamepata mafunzo maalum ya uongozi wa elimu na mbinu za kufundisha kimataifa, mpango utakaonufaisha wanafunzi 100,000 kutoka shule mbalimbali nchini.


Kozi hiyo ilitolewa na Taasisi ya The Robbin & Sylvia Goodall Foundation ya Uingereza kwa kushirikiana na Taasisi ya African Management Initiative ya Kenya na mwanzilishi wa shule hiyo kutoka Zanzibar, Shafii Haji.

Haji alisema kila alipokuwa akija Arusha kufuatilia maendeleo ya mafunzo hayo alikuwa akirudi nyumbani huku kichwa chake kikiwa ‘kimepasuka.’
“Programu hii imeleta mabadiliko chanya katika elimu,” alisema David Williams katika mahafali ya wahitimu hao yaliyofanyika jijini hapa jana.

Williams, Mwalimu Mkuu Mtendaji kutoka Uingereza aliyeandaa masomo katika kozi hiyo iliyoanza Januari mwaka huu, alisema amefurahishwa kuona ushirikiano kutoka serikalini na kwa washiriki, wanafunzi na jamii husika katika kipindi chote cha mafunzo  hayo.

Alisema walimu walipata nafasi ya kubadilishana uzoefu wa kazi kutoka maeneo yao na jumla ya wanafunzi 100, 000 kutoka shule mbalimbali nchini wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo.

Mkurugenzi wa Elimu wa taasisi hiyo, Lynn Thackway, amefurahishwa kuona walimu hao walivyopata mwamko wa kwenda kuleta mabadiliko ya elimu bora katika maeneo yao ya kazi.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Andrew Goodall, aliyeambatana na mama yake mzazi Sylvia, alisema uamuzi wa kuwekeza katika elimu nchini ni mapenzi yake ya dhati yeye na wafanyakazi wa taasisi hiyo  kwa Watanzania.

Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi na inatakiwa kuwa nchi ya kwanza Afrika kwa kuwa na uchumi mkubwa na imara, hivyo ameamua kutumia kozi hiyo kuelimisha walimu na wanafunzi kujua umuhimu wa rasilimali za nchi na kuzitunza.

Alisema elimu bora ndio msingi mkubwa kwa nchi katika kutunza rasilimali za nchi, hivyo basi taasisi yake imejikita katika kuboresha elimu na watu kujua umuhimu na kuzitunza.

Alisema alisikitishwa pale alipoona wanafunzi wanasoma kwa kukaa chini, chakula cha shida shuleni, umbali mrefu kutoka shule hadi nyumbani na ndio maana ameamua kutoa msaada wa madawati na kuzifanyia ukarabati shule zilizokuwa katika hali mbaya.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro, aliwataka walimu wakuu kuwa viungo kati ya walimu na serikali ili kutatua kero za walimu na kuboresha elimu kwa faida ya Watanzania.

Alisema kero zilizoko mashuleni  zinapaswa kutatuliwa na pande zote mbili za walimu wakuu kwa kushirikiana na serikali ili wanafunzi wapate elimu bora na kuiachia serikali pekee ni kuionea.

Aliwataka walimu mkoani hapa, kukubali kufanya kazi katika maeneo yoyote ya mkoa huku akikemea tabia ya baadhi ya walimu wakuu kutaka kufundisha mijini pekee.

Afisa Elimu Taaluma na Kaimu Afisa Elimu Wilaya ya Ngorongoro, Anyamisye Mahali, alisema mafunzo hayo yanaweza kubadilisha ufundishaji katika shule za msingi na wanafunzi kuwa na uelewa mpana kwa faida yao ya baadaye.

Mahali alisema ofisi yake itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wilaya hiyo inaongoza katika elimu mkoa na hata taifa.

No comments:

Powered by Blogger.