Yule shabiki wa Simba kuzikwa Moshi, Alhamisi
MWILI wa marehemu Shose Fidels Alhamisi utasafirishwa kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yaatakayofanyika Ijumaa.
Taarifa ya familia ya marehemu imesema kwamba mwili wa mpendwa wao,
Shose utaagwa mapema Alhamisi kabla ya safari ya kuelekea Moshi tayari
kwa maishi yake Ijumaa, ambayo yatafanyiak Uru.
Shose alifariki dunia Jumapili mchana, muda mfupi baada ya kufikishwa
hospitali ya mkoa wa Morogoro, kufuatia ajali ya gari aina ya Toyota
Land Cruiser V8 eneo la Dumila mkoani Morogoro.
Binti huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 na ushei, alikuwa
pamoja na Nahodha wa Simba, Jonas Mkude kwenye gari hilo na watu
wengine, wakitokea Dodoma, ambako jana timu yao ilitwaa Kombe la
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation
Cup (ASFC) kwa ushindi 2-1 dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Jamhuri.
Ndani ya gari hilo walikuwepo pia wapenzi wengine wa Simba, Jasmin na
Faudhia ambao wameumia na wamelazwa hospitali ya mkoa wa Morogoro na
hali zao zinaendelea kuimarika.
Mkude alirejeshwa Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi katika hospitali ya
Muhimbili kabla ya mapema Jumatatu kuruhusiwa, wakati dereva ambaye pia
ndiye mmiliki wa gari ajulikanaye kwa jina la utani, Rais wa Kibamba
anaisaidia Polisi.