Trump: Washirika wa Marekani katika Nato sharti walipe
Rais wa Marekani Donald Trump amewaambia washirika wa Marekani katika shirika la kujihami la mataifa ya Magharibi, Nato, mjini Brussels kwamba washirika wote ni lazima wagharimie sehemu yao ya gharama ya matumizi ya kijeshi.
Ni "kiasi kikubwa sana cha pesa" ambacho hakijalipwa, alisema, na kukariri wasiwasi ambao umekuwepo kwamba Marekani imekuwa ikilipa fedha zaidi kuliko washirika wake.
Bw Trump pia amelaani shambulio la bomu la Manchester lililotekelezwa Jumatatu na kusema kwamba ugaidi shari ukomeshwe.
Alitoa wito wa kuwepo kwa kipindi cha kimya kwa heshima ya watu 22, watu wazima na watoto, waliouawa katika "shambulio hilo la kikatili".
Bw Trump pia ameonya kuhusu hatari ambayo inaletwa na kuruhusiwa kwa watu kuhama bila kudhibitiwa na pia hatari inayotokana na urusi.
"Ugaidi ni lazima ukomeshwe au ukatili mlioshuhudia huko Manchester, na maeneo mengine mengi, utaendelea milele," alisema.
"Mna maelfu na maelfu ya watu wanaofurika na kuindia katika mataifa kadha na kuenea kote, na katika visa vingi hatuwafahamu hasa wao ni kina nani. Lazima tuwe wakali, lazima tuwe thabiti na lazima tuwe macho."
Kabla ya kuzuru makao makuu ya Nato, Bw Trump alikutana na viongozi kadha wa EU kwa mara ya kwanza, wakiwemo rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Nato itachukua hatua zaidi ili kuwashinda IS?
Marekani kwa muda mrefu imelaumu washirika wake wa Nato kwa kuchangia kiwango cha chini cha pesa za kutumiwa katika ulinzi, sana chini ya asilimia 2 ya mapato ya taifa, kiwango ambacho kimekubalika.
Nato wamekubali kutekeleza mchango mkubwa katika vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu, sana Islamic State, lakini Ufaransa na Ujerumani zimesisitiza kwamba hatua hii sana ni ya mdomo tu.
Katibu Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg amesema mataifa wanachama wa Nato yatasaidia kwa kupashana habari na kwa kuwezesha ndege za kivita kuongezwa mafuta zikiwa bado angani.
"Hili litatoa ujumbe mzito wa kisiasa kuhusu kujitolea kwa Nato kupigana dhidi ya ugaidi na kuimarisha ushirikiano na uhusiano wetu ndani ya muungano - lakini haina maana kwamba Nato itashiriki katika operesheni za kijeshi," amesema.
Kuna wasiwasi kwamba Nato ikijiunga na ubia wa mataifa yanayopigana na IS yakiongozwa na Marekani huenda hilo likapelekea muungano huo kujipata ndani ya mzozo wa baada ya vita Iraq na Libya kama ilivyofanyika nchini Afghanistan, anasema mwandishi wa BBC Jonathan Marcus.
Baada ya mkutano na Bw Trump mapema Alhamisi, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk alisema kwamba wameafikiana kuhusu mambo mengi lakini bado zipo tofauti kuhusu Urusi.
"Sina uhakika asilimia 100 kwamba tunaweza kuwa na msimamo mmoja kuhusu Urusi, ingawa kuhusu mzozo wa Ukraine, msimamo wetu ni mmoja," alisema.
Bw Trump ameshutumiwa kwa kuonekana kumuenzi Rais wa Urusi Vladimir Putin na hali kwamba utawala wake umekumbwa na madai ya kuwa na uhusiano wa karibu na maafisa wa Urusi.
Kabla ya kuzuru Brussels, Bw Trump alikuwa amezuru Israel na Maeneo ya Palestina baada ya kuanza safari yake ya kwanza nje ya Marekani Saudi Arabia.
No comments:
Post a Comment