Rasilimali (7) zinaweza kukupa mafanikio
Swali la msingi ni je tunazitumiaje rasilimali hizo kuwa fursa? Hapo ndipo palipo na changamoto kwa watu wengi. Na daima ukumbuke ule usemi mzuri usemao kuzaliwa Masikini si Kosa ila Kosa ni wewe kufa Maskini. Na kufa kwako maskini inategemea sana kwa kutokutumia vizuri rasilimali zifuatazo.
1.Uhai.
Katika zawaidi na rasilimali kubwa ambazo mwenyezi Mungu amekutunuku ni pamoja na uhai. Uhai ndiyo zawadi pekee ambayo ni vyema ukaitumia vyema katika maisha yako. Rasilimali hii ndiyo ambayo kila mmoja wetu anabidi aitumie vyema katika kubadili maisha yake. Kwanini ufe maskini na ili hali wewe u hai? Tafakari kisha tafuta majibu ya maswali yako.
Uhai huu tulionao hatuna budi tuutumie vyema, kwani mwenyezi Mungu ana makusudi ya dhati na sisi. Mwenyezi Mungu katupa uhai huu pasipo kutumia hata shilingi moja. Kama ndivyo hivyo naomba utafakari tena ni kwanini ufe maskini? . Uhai ulionao hakikisha unafanya kitu ambacho kitaacha alama duniani kote kabla hujarudi mavumbini.
2. Muda.
Muda ni rasilimali nyingine ambayo itakufanya wewe uweze kufikia ndoto yako endapo utaamua kutumia vyema muda ulionao. Katika hili ni vyema ukatenga kwa kila siku walau saa moja ambalo litakufanya uweze kufikiri ni jinsi gani utaweza kufikia vyema ndoto uliyonayo. Muda ni rasilimali kubwa sana ambayo watu wenye mafanikio huweza kuutumia kama silaha dhidi ya umaskini.
3. Akili.
Kila mwanadamu katika ulimwengu huu ana akili. Na akili hizi ndizo ambazo humtofautisha mtu mmoja na mwingine. Akili ndiyo msingi mkuu wa kumfanya mtu mmoja atofautie na mwingine. Akili ni njia ambayo itakufanya uweze kutimiza kusudio lako la kuwepo duniani hapa. Akili ndiyo rasimali tosha inayomfanya mtu afikiri nini afanye na nini asifanye. Hivyo nikusihi ifanye akili iweze kufikiri kabla ya kutenda, kwani changamoto kubwa ambayo inawafanya watu waweze kuwa maskini ni vile mtu anavyoamua "kutenda bila kufikiri" au "kufikiri bila kutenda'.
4. Nguvu.
Nguvu uliyonayo itumie vyema katika kutenda kazi mbalimbali. Lakini kutenda huku si kutenda tu, la hasha bali ni kutenda bidii. Kufanya kazi bila kuonyesha juhudi za maksudi ni sawa na bure.
5. Kipaji / talanta.
Rasimali nyingine uliyonayo inayoweza kukufanya uweze kufanikiwa ni kipaji. Watu wengi wenye mafanikio waliweza kutumia kipaji kwa asilimia kubwa, na leo tumeshuhudia ya kwamba mafanikio yamekuwa upande wao. Hivyo tumia talanta kama sehemu ya kukutoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Je kipaji ulichonacho kinakusaidia? Kama jibu ni hapana basi endelea kusoma mahali hapa kwani siku sijazo nitakueleza jinsi ambayo utaweza kugeuza kipaji hicho kuwa pesa.
6. Ardhi.
Ardhi pia ni sehemu ya maisha yako, kila kitu unachokitaka kukifanya lazima kiwe na mahusiano ya karibu na ardhi. Tafakari kwa umakini juu ya ardhi hii kisha uone fursa lukuki ambazo zimejificha katika ardhi, fursa hizo lukuki zitakusaidia kuweza kufanikiwa katika maisha yako.
7. Watu.
Rasilimali ya mwisho ambayo tutaijadili siku ya leo, ni kuhusu watu ambao wanakuzunguka. Kila kitu huwezi kufanya bila kushirikisha watu. Kama ni biashara inahitaji wateja, kama ni shule inahitaji wanafunzi, kama ni kanisa au mskiti nalo linahitaji watu pia.
Hivyo ni vyema ukaweza kuwatumia watu mbalimbali kuweza kufikia lengo lako. Kama unataka mfanyabishara tunachotegemea kuona kwako ni kuona rafiki zako wakubwa ni wafanyabishara wanzako.
"Kwani kuna usemi unao sema tutajie rafiki zako tujue tabia zako"
Hivyo hakikisha unazungukwa na marafiki wenye tija kila wakati.
Bila shaka umenielewa vizuri, kama umeshindwa kutumia vyema rasimali hizi basi "subiri kumshuhudia simba akila majani"
No comments:
Post a Comment