Trending News>>

WALENGWA WA TASAF MKOANI SINGIDA WABORESHA MAKAZI YAO KWA KUTUMIA FEDHA ZA RUZUKU.

Na Estom Sanga

Baadhi ya walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF mkoani Singida wameanza kuboresha makazi yao kwa kutumia sehemu ya fedha zinazotolewa na mfuko huo kwa njia ya ruzuku .

Wakizungumza na Waandishi wa Habari walioko katika ziara ya mkoa huo kuona namna walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini wanavyonufaika kupitia utaratibu wa uhawilishaji fedha,baadhi yao wamewaeleza waandishi hao kuwa licha ya kutumia sehemu ya fedha hizo kununua chakula na sare za watoto lakini pia wameweza kununua mabati na kuezeka nyumba zao na hivyo kuboresha makazi yao.

“nimeepukana na shida ya kuvuja kwa nyumba yangu baada ya kununua mabati na kujenga nyumba ya matofali kutokana na fedha za TASAF”amesema mzee shaaban Mkondya anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 70 mkazi wa eneo la Mtipa nje kidogo ya manispaa ya Singida.

Naye bi.Mwajuma Omary amewaeleza waandishi wa habari kuwa tangu aanze kupata ruzuku ya fedha kutoka TASAF mwaka 2014 hali yake ya maisha imeboreshwa na kuwa na walau uhakika wa kupata chakula huku akitumia sehemu ya fedha hizo kununua mabati 10 yaliyomwezesha kuezeka nyumba yake na hivyo kuboresha makazi yake.

“ninaishukuru TASAF kwa kutufikiria sisi wanyonge kama mimi kwani tulikuwa na hali ngumu ya maisha lakini sasa walau tunauhakika wa kupata fedha kila mwezi kulingana na utaratibu uliowekwa” amesisitiza Bi Mwajuma Omary mwenye umri wa miaka 77.

Kwa upande wake Mzee Jumanne kinda amesema utaratibu wa Serikali kupitia TASAF kuwafikia watu maskini umeamusha ari ya wananchi hao kujiletea maendeleo kwani sasa wanaweza kuanzisha shughuli za uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa kuku na mbuzi ili kujiongezea kipato.”nimeweza kununua mbuzi watano na kuezeka nyumba yangu kwa mabati kutumia fedha nilizozipata kutoka TASAF, ninawashukuru sana ,sikuwahi kufikiria kuishi kwenye nyumba ya bati “ amesisitiza Mzee Jumanne Kinda .

Hata hivyo licha ya mafanikio wanayoendelea kupata walengwa hao wa TASAF,wameeleza kuwa jitihada zao za kujikwamua na umaskini zimekuwa zikiathiriwa na magonjwa hususani yale yanaokumba mifugo hasa kuku wa kienyeji.

Wameiomba TASAF kuangalia namna inavyoweza kutoa motisha kwa wataalamu wa mifugo ili waweze kuwatembelea walengwa kwenye maeneo yao na kutoa ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kupunguza vifo vya kuku ambao hustawi vizuri mkoani Singida.

Zifuatazo hapo chini ni baadhi ya picha zinazoonyesha baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika manispaa ya Singida wakionyesha nyumba na mifugo walioipata baada ya kupokea ruzuku ya TASAF.


Sehemu ya mtaro uliojengwa katika eneo la Mtipa nje kidogo ya manispaa ya Singida kupitia utaratibu wa ajira ya muda unaotekelezwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini kupitia TASAF.
Mmoja wa walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini Mzee Shaaban Mkondya akiwa amesimama kando ya nyumba aliyoiezeka mabati kwa fedha za ruzuku ya TASAF na hivyo kuboresha makazi yake. 
Mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Mzee Shaaban Mkondya aliyesimama na mjukuu wake aliyevaa sare za shule akiwaonyesha waandishi wa habari nyumba yake ya zamani Kulia na ile mpya kushoto kwake aliyoezeka kwa mabati kwa ruzuku ya fedha za TASAF.
Bi. Mwajuma Omary (77) aliyeketi akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) nyumba yake mpya iliyoko kushoto kwake na kulia kwake ni nyumba yake ya zamani ikiwa katika mfumo wa tembe. 
Mzee Jumanne Muhiyo akizungumza na waandishi wa habari juu ya ujenzi wa nyumba yake mpya kwa kutumia fedha za ruzuku kutoka TASAF. 

Picha ya juu na chini inaonesha Mama wenye watoto chini ya miaka 5 wakiwa katika kituo cha afya cha Mtipa nje kidogo ya manispaa ya Singida wakitimiza moja ya sharti la Mpango wa kunusuru kaya masikini kuhudhuria kliniki. 

No comments:

Powered by Blogger.