WAZIRI MKUU AMALIZA MGOGORO WA MPAKA KILINDI NA KITETO
*Awaonya viongozi wa siasa wasiwavuruge wananchi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameumaliza mgogoro wa mpaka wa ardhi baina ya vijiji vya wilaya za Kiteto na Kilindi uliodumu kwa muda mrefu.
Mgogoro huo ambao ulianza kusuluhishwa tangu mwaka 1997, umepata suluhu kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu na kuwajumuisha Wakuu wa Mikoa hiyo miwili, Wabunge wa Kiteto na Kilindi, wenyeviti wa Halmashauri na madiwani wa kata mbili za mpakani pamoja na wananchi wa kata hizo.
Waziri Mkuu pia amewataka wanasiasa na viongozi wengine kutowavuruga wananchi na badala yake wawaongoze vizuri na kutoa maelekezo kwa mujibu wa sheria za nchi.Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Januari 18, 2017) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya za Kiteto na Kilindi katika kijiji cha Lembapili wilayani Kiteto, mkoani Manyara ambako ni kuna mpaka wa wilaya hizo mbili alipokwenda kutatua mgogoro huo.
Amesema viongozi wa wilaya hizo lazima wafuate sheria na wawaelekeze wananchi umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuheshimu mipaka iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ili kuepusha migogoro.
Akizungumzia kuhusu mgogoro huo wa mpaka, Waziri Mkuu amesema nchi ilishaweka mipaka ya mikoa na wilaya zake yote tangu zamani na kumbukumbu zipo zikiwemo za mpaka wa wilaya hizo tangu mwaka 1961 kwa tangazo la Serikali namba 65 na hakuna mabadiliko. Hivyo, aliwasisitiza wauheshimu na kuufuata.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itakwenda kuweka alama vizuri na viongozi wa wilaya hizo watashirikishwa. Alama hizo zitawekwa na kifaa maalumu, hivyo amewataka wahusika watoe ushirikiano.
Waziri Mkuu amesema katika kipindi ambacho Serikali itakuwa ikiweka alama hizo, wananchi waendelee na shughuli zao hadi hapo zoezi litakapokamilika na wala wasibughudhiwe.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa siku nane kwa watu wote wanaomiliki silaha katika wilaya za Kilindi na Kiteto wazipeleke kwenye vituo vya Polisi ili zisajiliwe upya na kisha Wakuu wa Mikoa wafanye operesheni maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume cha sheria achukuliwe hatua.
“Wakuu wa Mikoa fanyeni ukaguzi maalum na atakayekutwa anamiliki silaha kinyume na utaratibu achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria. Pia kuna watu wana mitambo ya kutengenezea bunduki hapa, nao pia waisalimishe haraka,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi amesema mwanzoni mwa Februari wataalamu wake watakwenda katika mpaka huo ili kuanza kuweka alama vizuri.
Amesema baadhi ya viongozi huwa wana tabia ya kuzuia watendaji kutekeleza majukumu yao, hivyo ametumia gursa hiyo kuwaomba viongozi wa wilaya hizo watoe ushirikiano.
Amesema moja ya majukumu aliyopewa na Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli ni kuhakikisha ndani ya miaka hii mitano anamaliza migogoro ya ardhi nchini ukiwemo huo wa Kilindi na Kiteto.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, JANUARI 18, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizugumza na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera wakiwa katika kijiji cha Lembapuli kilichopo kwenye mpaka wa wilaya ya Kiteto na Kilindi Januari 18, 2017. Mheshimiwa Majaliwa alikwenda Kiteto na Kilindi kutatua mgogoro wa mpaka unaovikabili vijiji vya Mafisa na Kijungu. Wapili kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Muu wa Wilaya ya Tanga mjini , Thobias Mwilapwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akielekea kwenye moja ya jiwe la mpaka wa wilaya ya Kilindi na Kiteto wakati alipokwenda kwenye kijiji cha Lembapuli kilichopo kwenye mpaka wa Kiteto na Kilindi kutatua mgogoro wa mpaka Januari 18, 2017. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera na kulia kwake ni Mkuu wa wilaya na Tanga na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga Thobias Mwilapwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa watalaam wa upimaji ardhi kuhusu jiwe la alama ya mpaka wa wilaya ya Kilindi na Kiteto katika kijiji cha mpakani cha Lembapuli Januari 18, 2017. . Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera na kulia kwake ni Mkuu wa wilaya na Tanga na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga Thobias Mwilapwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kuhusu ramani inayoonyesha mpaka wa wilaya ya Kilindi na Kiteto katika kijiji cha mpakani cha Lembapuli wakati alipokwenda kutatua mgogoro wa mpaka kati ya wialya hizo Januari 18, 2017. Mheshimiwa Majaliwa apia alifuatana na Mawaziri , William Lukuvi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi na George Simbachawene wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wa Kiteto na Kilindi wakati alipokwenda kwenye kijiji cha Lembapuli kilichopo kwenye mpaka wa wilaya hizo kutatua mgogoro wa mpaka Januari 18, 2017. Wapili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera na wapili kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutanao wa hadhaa katika kijiji cha Lembapuli kilichopo mpakani mwa wilaya za Kilindi na Kiteto alikokwenda kutatua mgogoro wa mpaka Januari 18, 2017.
Baadhi ya wananchi wa wilaya za Kilindi na Kiteto wakimshangilia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Lembapuli kilichopo mpakani mwa wilaya za Kiteto na Kilindi alikokwenda kutatua mgogoro wa mpaka Januari 18, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment