Trending News>>

Ukiona anang’ang’ania mapenzi ya siri, ujue ana lake jambo



Uhali gani mpenzi msomaji, leo utakuwa nami, Lulu Diva, wengi wananifahamu kwa sababu ya kazi yangu ya uanamitindo, na msanii wa filamu za Kibongo na Bongo Fleva, leo nataka nizungumze nawe msomaji kuhusu mambo yahusuyo mapenzi.



Kuna baadhi ya watu, wamekuwa na kawaida ya kutaka mapenzi yao yawe ya siri. Umewahi kusikia au kushuhudia watu wawili wanaopendana, wakiendesha uhusiano wao kwa siri kubwa?


Najua wapo wengi ambao wapo kwenye uhusiano wa siri na wanazo sababu zinazowafanya waishi kwenye aina hiyo ya uhusiano, lakini je, kama unampenda, na yeye anakupenda kwa dhati, kuna haja gani ya kuishi kwenye uhusiano wa siri? Ukiona mtu anang’ang’ania mapenzi ya siri, ujue ana lake jambo na inawezekana ikawa ni miongoni mwa nitakayoyataja.


Yawezekana umejikuta tu katika mkumbo wa mapenzi ya siri! Yaani mwenzi wako ndiye anayekulazimisha muishi aina hiyo ya maisha lakini ndani ya moyo wako unaona kama unaidhulumu nafsi yako.


Unatamani kila mtu ajue kwamba ninyi ni wapenzi lakini mwenzi wako anakukataza kufanya hivyo. Pengine hata anakupa vitisho kwamba utakapotoa siri ya uhusiano wenu, huo ndiyo utakuwa mwisho wa mapenzi yenu.


Shtuka! Chunguza kwa kina kwa nini mwenzi wako anataka muishi maisha ya mapenzi ya siri wakati kila siku anakwambia kwamba anakupenda na yupo tayari kufanya chochote kwa ajili yako.


Sababu kubwa ya kwanza inayowafanya wengi wapende kuwa na uhusiano wa siri na wenzi wao ni kwa sababu wanakuwa wapo kwenye ndoa halali lakini kwa sababu ya tamaa zao, wanaamua kuchepuka. Katika kuchepuka huko, hawawaambii wenzi wapya ukweli kwamba tayari wanao wake au waume zao halali.


Wanawadanganya kwamba wapo singo ili wawatumie kimapenzi na watakapomaliza haja zao ndiyo wawaeleze ukweli na kuvunja mapenzi yao. Upo ushahidi wa wanawake wengi ambao walitongozwa, wakakubali kuanzisha uhusiano wa siri na wanaume na kukaa nao kwa kipindi kirefu lakini baadaye wakaja kugundua kumbe wao ni ‘spea tairi’.


Vilevile wapo wanaume ambao wameingizwa mkenge kwa kuingia kwenye uhusiano wa siri na wanawake, wakiwahudumia na kuwatimizia kila kitu lakini kumbe nyuma ya pazia ni wake za watu.


Sababu nyingine inayosababisha wengi wapende kuishi na wenzi wao kwa usiri, ni tabia ya umalaya au uhuni anayokuwa nayo mtu. Kwamba katika sehemu hiyohiyo moja, wewe unadhani uko peke yako lakini kumbe kuna wenzako kadhaa unapanga nao foleni. Kwa kuwa kila mmoja anatunza siri, inakuwa vigumu kujuana.

Bila shaka umenielewa, kwa hiyo ni suala la kujiongeza tu, kuwa makini.

No comments:

Powered by Blogger.