AJIRA:Walimu wa sayansi wapya wapewa muda wa mwisho
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa fursa ya mwisho kwa wahitimu wa ngazi za Stashahada na Shahada za ualimu ambao hawakuwasilisha vyeti vyao kwa ajili ya uhakiki kufanya hivyo kabla ya Januari 17.
Uhakiki wa vyeti kwa wahitimu wa ngazi za Stashahada na Shahada za ualimu katika masomo ya Sayansi ambayo ni Fizikia, Kemia na Bayolojia pamoja na masomo ya hisabati wa mwaka 2015 ulitangazwa na wizara hiyo mwishoni mwa mwaka jana.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari alieleza, baadhi ya wahitimu walituma nyaraka zao zikiwa na mapungufu hivyo na wao wanapaswa kuziwasilisha upya.
Alisema kwa wahitimu wanaopaswa kuwasilisha upya ni wale ambao walituma nyaraka za matokeo ya mtihani (Results Slips) au matokeo Academic Transcript bila nakala za vyeti halisi vya kidato cha nne, sita au Shahada.
Wengine ni waliotuma nakala za vyeti vya Stashahada za Uzamili bila nakala za vyeti vya Shahada ya Kwanza pamoja na matokeo yake elimu (Academic Transcripts).
“Wahitimu ambao hawakutuma kabisa nakala za vyeti wanapewa fursa ya mwisho kutuma. Wahitimu ambao nyaraka zao ziliwasilishwa kikamilifu na kupokelewa, majina yao yamewekwa kwenye tovuti ya wizara,” alisema Profesa Msanjila.
Akitoa ufafanuzi kuhusu utaratibu wa kutuma vyeti alisema, waombaji ni lazima watume vivuli vya vyeti halisi vya kidato cha nne, cha sita, Stashahada na Stashahada ya Uzamili au Shahada na siyo kivuli cha cheti.
Aidha, waombaji wa Stashahada ya Uzamili na Shahada ni lazima watume vivuli vya matokeo ya Shahada za kwanza na pia waombaji lazima waweke nakala hizo katika faili moja lililo katika mtindo wa PDF na kupewa jina la mwombaji husika.
Profesa Msanjila alisisitiza kuwa waombaji wanapaswa kutumia baruapepe zao wenyewe na sio za watu wengine.
Alitaka maombi hayo kutumwa kupitia baruapepe ya wizara ambayo ni info@moe. go.tz. Hatua hiyo ya uhakiki wa vyeti vya wahitimu hao ilikuwa ni kwa ajili ya uchambuzi wa wahitimu wenye sifa.
ManyamaJr
No comments:
Post a Comment