Yanga Pemba, Simba Kambi Moro
WAKATI Simba SC inatarajiwa kwenda kuweka kambi Morogoro wiki hii, mahasimu wao Yanga wao wamepanga kwenda Pemba wakati wowote kuanzia leo.
Timu zote zinajiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na tangu wiki iliyopita zimeanza kambi zake za muda za mazoezi mjini Dar es Salaam.
Yanga walianzia Uwanja wa Chuo cha Maofisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini, Dar es Salaam Jumatatu iliyopita kabla ya Jumatano kuhamia Uwanja wa Gymkhana, Jijini.
Mahasimu wao, Simba tangu Jumatano wanafanya mazoezi yao Uwanja wa Chuo cha Maofisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini, Dar es Salaam pia. Na ikumbukwe Yanga waliamua kuondoka Chuo cha Maofisa wa Jeshi la Polisi, baada ya watani wao, Simba nao kuhamia hapo.
Pamoja na hayo, kocha mpya wa Yanga, Mzambia George Lwandamina anataka mchezo mmoja wa kirafiki haraka ili kuwajua vizuri wachezaji baada ya kurithi timu kwa Mholanzi, Hans van der Plujim mwezi uliopita. Pluijm sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi.
Haijulikani kama mchezo huo utakuja kabla au baada ya kambi ya Pemba, lakini kwa leo Yanga wataendelea na mazoezi Uwanja wa Gymkhana.
Kwa Simba, kocha Mcameroon Joseph Marius Omog anaonekana kuvutiwa zaidi na kambi ya Morogoro baada ya kujificha huko kwa maandalazi ya mwanzoni mwa msimu na amependekeza timu irudi huko.
Uongozi wa Simba SC unataka kuharakisha kuingia mikataba na wachezaji wapya na ambao wamemaliza ndani ya siku mbili hizi ili timu iwahi kwenda kambini Morogoro.
Ikumbukwe Simba SC walimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu wakiwa wanaongoza kwa pointi zao 35, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga.
No comments:
Post a Comment