WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AFUNGUA KITUO CHA TAALUMA YA UHASIBU (NBAA) BUNJU
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA) kuwachukulia hatua wale wote wanaoitia doa taaluma hiyo kwa kufanya ubadhilifu wa fedha za umma.
Maagizo hayo yametolewa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango, wakati wa Uzinduzi wa Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC) uliokwenda sambamba na ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa wahasibu unaojumuisha wadau kutoka nchi za Afrika Mashariki, katika eneo la Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Amesema kuwa Idadi ya Wahasibu wenye sifa inazidi kuongezeka na hivyo kuisaidia Serikali, japo kuwa Serikali hairidhiki kuona wanataaluma wa Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu (CPA) wanaongezeka huku vitendo vya ubadhilifu wa fedha za Umma na ufisadi vikiendelea kuripotiwa.
“Wapo hata wahasibu wanaotumia taaluma yao vibaya, wanaowawezesha wafanyabiashara kukwepa kodi, wanachakachua vitabu vya taarifa za fedha na kufanya ufisadi kwa njia ya kalamu na kompyuta jambo ambalo halikubaliki hata kidogo” Aliongeza Dkt. Mpango
Amesema kuwa machozi ya masikini wa Tanzania yatawafuata mafisadi hadi kaburini lakini serikali ya Awamu ya Tano haitasubiri hao mafisadi wafe, itawatumbua na wala hakuna mzaha na kwamba tayari mahakama ya mafisadi imeanza kazi na itawashughulikia.
Aidha, Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewaasa wanataaluma wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu kuitumia taaluma yao kuisaidia Serikali katika hatua yake ya kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda kwa kuwa taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu, Bw. Pius Maneno amesema kuwa, Kituo hicho kilichozinduliwa cha APC hadi kumalizika, kitagharimu Sh. Bilioni 35 ambapo mpaka sasa fedha zilizotumika ni takribani Sh. Bilioni 33
“Gharama halisi za ujenzi wa kituo hicho zilikuwa Bilioni 14 lakini kutokana na mzabuni wa ujenzi kuchelewesha ujenzi ndio maana kumekuwa na Ongezeko la kiasi hicho cha fedha” aliongeza Bw. Maneno.
Ujenzi wa kituo hicho ambao uko katika eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 14 umehusisha ujenzi wa Kumbi za mikutano zinazochukua zaidi ya watu 1600, viwanja vya michezo na vyumba vya kisasa 108 vya kulala wageni.
Bw. Maneno amesema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutaifanya Bodi hiyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kikitumika kukodi kumbi za kufanyia na kusahisha mitihani ya Bodi (NBAA).
Amezitaja faida zingine kuwa ni kuboreshwa kwa mazingira ya kitaaluma na wanataaluma wa uhasibu pamoja na kuimarika kwa utawala bora na kuwa chachu ya uchumi wa viwanda, kwa kuwa Kituo hicho, kinatoa elimu bora itakayowawezesha wahitimu kuingia kwenye ushindani ndani ya nchi za Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla.
Ujenzi wa Kituo hicho umedhaminiwa na serikali kupitia mkopo kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii-NSSF, Bodi ya Uhasibu-NBAA na Mbia mwenza wa kituo hicho, Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali-GEPF.
Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango (kulia), akikata utepe kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuashiria kuzindua rasmi Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC), kilichopo Bunju jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Profesa Isaya Jairo na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa GEPF, Joyce Shaidi.
Mwonekano wa baadhi ya majengo ya kituo hicho.
Mwonekano wa ukumbi wa mikutano wa kituo hicho.
No comments:
Post a Comment