Trending News>>

VIJANA NCHINI KUFUNDISHWA UTENGENEZAJI VIFAA VYA UMEME WA JUA..


Na Teresia Mhagama 
Vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini watafaidika na mafunzo yatakayotolewa na kampuni ya Empower kutoka Korea yatakayohusu utengenezaji vifaa Umeme Jua ambavyo vinatumika kuwasha taa na kuchaji simu huku gharama yake ikiwa ni nafuu. 
Hayo yamebainika jijini Dar es Salaam wakati wa kikao baina ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Balozi wa Korea nchini, Song  Geum-Young  na watendaji wa kampuni ya Empower, inayotengeza vifaa hivyo. 
Watendaji wa kampuni hiyo  walifika na baadhi ya vifaa hivyo vya Umeme Jua ili kuionesha Wizara namna vinavyofanya kazi. 

Dkt. Hong Kyu Choi, kutoka kampuni ya Empower alisema kuwa wamepanga kutoa mafunzo hayo sehemu mbalimbali nchini ili vijana hao waweze kujiajiri na pia kuwezesha wananchi hasa wa vijijini kupata huduma ya umeme. 
Alisema kuwa mafunzo hayo pia yatatolewa kwa walimu wa Sayansi nchini ili nao waweze kuwafundisha wanafunzi kuhusu teknolojia na hivyo kuwa endelevu. 
“ Vijana wa Tanzania wana uelewa mkubwa sana hivyo wanachohitaji ni kupata fursa ya kupata mafunzo kama haya na nyenzo ili waweze kujiajiri na pia kuweza kufundisha watu wengine, hii itawasaidia wao kujiajiri pia,” alisema Dkt. Choi. 
Kwa upande wake, Profesa Muhongo alisema kuwa vifaa hivyo ni muhimu sana hasa katika sehemu ambazo hazijafikiwa na nishati ya umeme na kwamba suala la kutoa mafunzo hayo kwa vijana ni muhimu kwani itawawezesha kupata uelewa wa teknolojia inayotumika kutengeneza vifaa hivyo pamoja na  kujiajiri. 
“Napata simu nyingi sana Watu wakilia, Umeme, Umeme, hii teknolojia ni nzuri na itawasaidia wananchi wetu kupata mwanga na pia kuchaji simu zao, hivyo nawakaribisha kuanza kutoa mafunzo hayo mwezi Machi mwakani,” alisema Profesa Muhongo. 
Hii ni mara ya Pili kwa Profesa Muhongo kukutana na Watendaji wa kampuni hiyo ambapo mara ya kwanza alikutana nao mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu ambapo Balozi wa Korea hapa nchini alifika kuitambulisha kwa Waziri wa Nishati na Madini na pia kueleza shughuli za kampuni hiyo katika sehemu mbalimbali duniani. 
Katika Kikao hicho cha mwezi Novemba, Mtendaji wa Empower, Dkt.  Choi alisema kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikitengeneza vifaa hivyo vya Umeme Jua kwa kutumia teknolojia ya kisasa tangu mwaka 2011 na kwamba lengo lake ni kusambaza huduma hiyo vijijini ili kuwasaidia vijana na wananchi kupata huduma ya umeme na  kwa gharama nafuu. 
Alitaja baadhi ya kazi ambazo wameshazitekeleza kuwa ni pamoja na kubuni na kutengeneza Mfumo wa Umeme Jua katika Kituo cha ‘City Christian Center (CCC)’ kilichopo Dar es Salaam pamoja na kutengeza Paneli za Umeme Jua za gharama nafuu katika  sehemu mbalimbali Barani Afrika. 

Aliongeza kuwa gharama ya Paneli hizo ni nusu ya bei ya kuunganisha umeme unaosambazwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao unagharimu shilingi 27,000 .
Posted By Manyama EJG.

No comments:

Powered by Blogger.