Trending News>>

SIMULIZI YA KUSISIMUA NA KUBURUDISHA

SIMULIZI: DOKTA SIUMWI HUKO
SEHEMU: YA TISA
MTUNZI: Mr ManyamaJr
MAWASILIANO: 0767464766


ILIPOISHIA:
"Kesho uje unipitie nyumbani jioni ya saa moja na nusu, sawa?"
"Saa moja na nusu?," Monica alihoji kwa mshangao mkubwa.

WEWESEKA NAYO SASA
Ee, saa moja jioni ndiyo, mbona unashituka Monica?," Sulee alihoji kwa sauti ya kishari f'lani hivi.

"Mmh!, nimeshangaa muda huo ni daktari gani anatoa huduma ya tiba kwa uzazi!"
"Kha! Monica vipi kwani wanaojifungua huwa hawaendi kuzaa usiku?"

"Umeshasema kujifungua, sasa mimi naenda kujifungua?" alisema Monica huku akitingisha mguu mmoja na kulifanya wowowo lake litikisike kwa kitetemeshi cha kuvutia

"Kama unataka tiba, utakuja nikupeleke na kama hutaki basi bwana nimeshaona una wasiwasi," alisema Sulee akijiandaa kuondoka.

"Hapana shoga yangu, nitakuja bwana"
"Oke, utanikuta ila usichelewe"
"Sawa shoga yangu"

Waliagana lakini moyoni Monica akabaki na maswali yasiyokuwa na majibu.

"Saa moja na nusu jioni tiba gani ya uzazi hiyo?"

"Lakini kwani tiba huwa ina muda maalum, na mimi bwana!"
"Lakini ngoja, sasa hiyo saa moja na nusu kuna kuwa na wagonjwa wengine?"

"Ee, sasa si pale ni hospitalini?"
"Mmh! Itajulikana hukohuko kesho;," Monica alizidi kuwaza na kuwazua moyoni mwake.

Kesho yake Monica aliamka mapema asubuhi na kuanza kufanya kazi ndogondogo za pale nyumbani. Hamu kubwa ni kufika muda alioambiwa na Sulee wa kwenda kumuona Dokta Kisarawe.

Ilikuwa mara aingie jikoni, mara sebuleni wakati mwingine mara aguse hiki na kuacha kile. Lengo likiwa ni kusukuma muda.

Saa kumi na mbili kamili jioni, Monica alijiandaa vizuri. Akaingia bafuni na kujisafisha kwa umakini mno. Hata maeneo ambayo hakuwa ameyasugua kwa muda mrefu, siku hiyo aliyaosha kwa ustadi.

Kuanzia ndani ya kucha za miguuni, katikati ya vidole na kwingineko, ilimradi tu aonekane bomba zaidi.

"Hapa sasa ngoja nikajipigilie pamba za maana," Monica aliwaza wakati akimalizia kujifunga taulo kabla ya kutoka bafuni

Aliingia chumbani kwake na kuanza kuchambua nguo zote alizozipenda. Kila aliyoijaribisha aliona kama haikumfaa kwa siku hiyo

"Eehee, hii ndiyo nilikuwa naitaka sasa ngoja niitupie" alisema Monica na kuiweka pembeni nguo hiyo.

Lilikuwa gauni jekundu, lakini lilibana sana maeneo ya nyuma na kuufanya mzigo wa Monica ujitenge vizuri kila alipolivaa. Kwenda chini lilikomea chini kidogo ya magoti

Alipojiridhisha, alifungua droo ya upande wa kitanda na kutoa pafyumu kali aina ya Red door, ambayo hutumiwa na wanawake wengi wa mjini ambao mambo yao yako bomba.

Akachukua sendozi za rangi nyeusi na kumechishia na mkoba wake, hakika alitokelezea kama wasemavyo vijana wa siku hizi.

Saa moja na nusu jioni, tayari Monica alikuwa sebuleni kwa Sulee akimsubiri waende kwa Dokta Kisarawe.

"Nimekuweka sana shoga yangu?"
"Wala usijali, tayari?"
"Eee, twende sasa;"

Waliongozana hadi kwa Dokta Kisarawe. Walipofika walikuta dokta huyo akimalizia kutoa maagizo fulani kwa mgonjwa mmoja.

Baada ya muda mfupi, Sulee alimpeleka Monica kwenye chumba cha daktari.

Dokta Kisarawe baada ya kumuona tu Monica, alishituka kwa uwazi na kuwafanya wote wauone mshituko huo.

"Ooh, karibuni sana;," alisema Dokta Kisarawe huku akijiweka sawa kwenye kiti chake kirefu cha kuzunguka.
"Ahsante," aliitikia Sulee kwa sauti ya uchangamfu.

Baada ya utambulisho, Dokta Kisarawe alimuomba Sulee awaache na Monica ili aweze kumsikiliza kwa umakini mkubwa.

Sulee alitoka nje na kukaa kwenye benchi, lakini moyo na akili yote vikabakia chumbani kwa Dokta Kisarawe na Monica.

Kilipita kimya kidogo bila kusikia sauti yoyote achilia mbali minong'ono;

Akaendelea kukaa huku akijiuliza maswali.

"Sasa mbona sisikii wakiongea?"
"Au mh..." Sulee hakumalizi sentensi yake na kuishia kuguna.

Kimya kikazidi kupita. Giza nalo likazidi kutanda, lakini hakuwa na jinsi zaidi ya kuendelea kumsubiri Monica aliyekuwa akipata tiba maalum.

Kuna wakati alitamani avamie ndani ili kuona kilichokuwa kinaendelea kati ya Dokta Kisarawe na rafiki yake Monica, maana tayari alishaanza kuhisi wivu f'lani hivi hasa akikumbuka jinsi yeye alivyoanzisha uhusiano na Dokta Kisarawe.

Wakati akiwaza hili na lile, ghafla alishituka baada ya kusikia kitu kama meza au kitanda kikilia kuashiria kama kuna mtu anakisogeza.

Akanyanyuka alipokuwa amekaa na kwenda hadi mlangoni.

Kwa kutumia tundu la komeo la mlangoni, Sulee alichungulia ndani.

"Duh! Yaani kweli?" Sulee alitamka maneno hayo baada ya kuona kwa ndani.

JE UNAHISI SULEE AMEONA NINI NDANI HADI IKAMFANYA ASHITUKE?
 NINI KITAENDELEA USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

No comments:

Powered by Blogger.