SIMULIZI FUPI "PENZI LENYE DHARAU"
MTUNZI MANYAMAJR EJG.
Sikujua kwanini alikuwa ananicheka kwani jambo nililokuwa namueleza lilikuwa ni la muhimu sana, niliendelea kuzungumza bila ya kujali kuwa alikuwa akinicheka "Hiki ninachokueleza ni kitu cha muhimu sana katika maisha yangu na yako, kwasababu nimeona tumekuwa katika uhusiano kwa miaka mitatu sasa. Lakini kila nikikuuliza nini malengo ya mapenzi yetu umekuwa ukiniambia kuwa nisiwe na wasiwasi kwani una malengo mazuri na mimi, sasa mimi nakuambia kuwa natamani sikumoja tufunge ndoa na kuishi pamoja milele, wewe unacheka bila ya kujibu chochote nashindwa kukuelewa Tina".
Aliongea George ambaye alikuwa amesimama huku akimtizama Tina aliyekuwa akicheka sana. Kijana huyu alikuwa akimpenda sana Tina kiasi kwamba alikuwa yupo tayari kwa lolote juu yake na mapenzi yao yalikuwa yakienda vizuri kwa takribani miaka mitatu. Ilifikia kipindi George alimtambulisha Tina kwa wazazi wake. Lakini kila alipokuwa akimtamkia suala la kutaka kufunga ndoa Tina alikuwa akimuambia kuwa asubiri, kwani mambo mazuri hayahitaji haraka. Kwa wakati huo Tina alikuwa anafanya kazi kama katibu muhitasi katika kiwanda cha sabuni, na George alikuwa ni mfanyabiashara.
Baada ya George kuona kuwa amekuwa akimuomba Tina wafunge ndoa bila mafanikio. Ilifikia kipindi akaamua kunyamaza kimya na kumuacha Tina afikirie, na akifikia muafaka basi atampa jibu. Maisha yaliendelea, Huku Tina akionekana kubadilika sana, na wakati mwingine alikuwa akimdharau sana George. Sikumoja walikuwa wametoka pamoja yapata majira ya saa moja jioni, walifika katika mgahawa mmoja na kuketi, wakiwa pale alikuja dada mmoja anaendesha gari aina ya Rav 4, dada huyu alikuwa akifahamiana na Tina alishuka kwenye gari yake na alipomuona Tina moja kwa moja alijisogeza na kumsalimia.
Ndipo Tina alipoamua kumtambulisha George nakusema "Joyce huyu ni rafiki yangu anaitwa George, karibu tujumuike pamoja, na pia unaweza kutusaidia lifti kwani huyu mwanaume hana hata gari la kusingiziwa, sijui hata anasubiri nini kununua gari yaani mwanaume suruali tu, tizama mwanamke anakuwa na gari zuri, na mwanaume kama huyu anajitutumua kuwa anataka kunioa, hata bajaji hana"
Aliongea Tina huku akiwa anamtizama George kwa dharau, na Joyce alitabasamu na kusema "Mh wewe Tina, mbona una maneno machafu kiasi hicho, haya bwana mimi siyo mkaaji nimekuona tu nikaamua kuja kukusalimia, kuna sehemu nakwenda."Aliongea Joyce huku akiwa anaondoka na wakati huo George alikuwa amenyamaza kimya huku moyoni akiwaza "Hivi, kweli mimi naweza kudharaulika kiasi hiki tena mbele za watu, Mungu wangu huyu mwanamke ana tabia mbaya sana, sijui nimpige, hapana ngoja nimuache kwasababu nikimpiga naweza kumvunjavunja ikawa kesi nyingine" Alikuwa anawaza George huku akionekana kuwa na hasira kali sana lakini alijaribu kuzuia hisia zake, na moja kwa moja alimgeukia Tina nakusema.
"Asante sana Tina kwa maneno yako ya dharau, mimi si lolote na si chochote kwako sasa nimelifahamu hilo usijali, nitakuacha uendelee na maisha yako, ila kumbuka nilikupenda sana lakini nilichoambulia kwako ni dharau asante sana" Aliongea huku akinyanyuka na kuondoka, Tina alisimama na kuanza kucheka "Hahahahahah kwenda zako, nani aolewe na wewe, mimi mwanamke mzuri bwana, nahitaji matunzo wewe una nini, huwezi hata kuninunulia gari, kwenda zako" Alioongea Tina bila ya kujali kama kuna watu wanamtizama. George aliondoka kimya bila hata ya kugeuka nyuma. Maisha yaliendelea na sasa George na Tina walitengana. Baada ya miezi saba kupita George alipata mchumba ambaye alimpenda sana katika shida na raha na walifunga ndoa huku wakiishi maisha yaliyojaa upendo, walishirikiana katika kila jambo.
Mungu aliwajalia Biashara ziliwaendea vizuri hivyo walianza kufanikiwa. Walijenga nyumba na baadaye walinunua magari, ambapo kila mmoja alikuwa akiendesha gari lake. Mungu aliwajalia wakafanikiwa pia kupata watoto wawili ilikuwa ni familia iliyojaa upendo. Kwa wakati wote huo George hakuwahi kuwasiliana na Tina hadi sikumoja ambao alikuwa akiendesha gari lake, na akiwa njiani alikutana na mwanamke mmoja ambaye alikuwa amejitanda kanga mbili dada huyu alikuwa akinyoosha mkono kuomba lifti ndipo George alisimamisha gari na kutaka kumuuliza kuwa alikuwa anaelekea wapi, alipofungua vioo vya gari alikutana uso kwa uso na Tina aliyeonekana kuchoka sana na usoni alikuwa ana vipele vingi.
Kwa namna alivyokuwa anaonekana alikuwa ni mgonjwa, mwanzoni George alfikiri amemfananisha ndipo alipomuita jina lake, Tina alibaki ameduwaa kwani hakutegemea kukutana na George akiwa anaendesha gari zuri aina ya Prado, alitaka kusita kupanda kwenye gari lakini George alimsisitiza apande ili amsaidie kumpeleka hospitali.
Wakiwa njiani Tina alikuwa akilia sana huku akisema "Naomba unisamehe, George, dunia imenifundisha, kwani niliolewa na mwanaume tajiri, kumbe yule mwanaume alikuwa ni muuza madawa ya kulevya, alikamatwa na ameniachia watoto watatu, hatuna chochote, mali zote zimechukuliwa, hapa nilipo ni mgonjwa, nimeathirika na virusi vya Ukimwi naishi kwa matumaini, inaniuma sana nikikumbuka nilivyokutenda, nisamehe George" Aliongea Tina huku akilia sana kwa uchungu, George alimtizama na kumuonea huruma sana "Usijali Tina mimi nimekusamehe toka siku nyingi sana, Mungu atakusaidia." Alimpeleka hadi Hospitali kisha alimsaidia pesa kidogo kwaajili ya matumizi.
FUNZO
Katika maisha unaambiwa dharau ni mbaya sana na siku zote kumbuka unapomfanyia mtu ubaya, ipo siku utajuta, kwani malipo ni hapahapa Duniani.
No comments:
Post a Comment