Shoga: tui la nazi lazima lionjwe!
SHOGA yangu u hali gani? Ni Jumanne nyingine tena tulivu imefika na tumekutana kwenye kona yetu hii inayowaelimisha wengi hususan wanawake wenzangu japo wanaume nao siwaachi nyuma. Natumai na wewe ni mzima wa afya na kama mgonjwa nakuombea kwa Mwenyezi Mungu atakutia nguvu.
Baada ya hayo tugeukie basi kwenye hiki kilichonifanya niwaandikie, si mnakumbuka mara ya mwisho nilitoa somo la chakula cha usiku hakifunikiwi!
Wengi mlinipigia simu na kunitumia meseji jinsi mnavyowafanyia waume zenu. Inanipa raha sana kuona mada imewaingia kisawasawa na kuyafanyia kazi shoga, mwanamke sharti ujue kukipika chakula bwana!
Kiwe kitamu pia usimfunikie mume wako eti kwa kuhofia nzi au kupoa, kifunue ili akila ajihisi ameridhika, upo?
Shoga baada ya hayo, nimepata maswali mengine mengi kutoka kwa nyie wasomaji wangu wengi mnaniuliza hivi tui la nazi lina utamu gani? Wengine mnauliza kwani lazima lionjwe? Jamani hata hili kweli la kuuliza au la kujiongeza mwenyewe? Umeshaandaa mboga yako, nazi ukune mwenyewe, machicha ukamue mwenyewe eti kuonja unataka usaidiwe. Tui la nazi sharti lionjwe shoga, usiwe zoba utaibiwa mjini, ahii!
Wengine wanaishia kuonja machicha tu, wanashindwa kumalizia kupata utamu wa tui lenyewe, wanashindwa kujua hata tui la kwanza na la pili lipi tamu. Nikupashe tu shoga, wanaume wa sasa ni wa kimjinimjini, wakizunguzungu tena wengine wakichinachina!
Chunga sana siku hizi kwani wanawake wengine wanaweza kumnasa mwandani wako na wakamuandalia tui, balaa itakuja kama tui hilo litakuwa zito kuliko unalopika wewe, mume akiona hilo ni tamu anaweza kukuhama. Wengi wazembe wamewahi kukimbiwa na waume au wapenzi wao kutokana na kupika tui jepesi na kutokuwa na ladha!
Unapoandaa tui la nazi yako jitahidi liwe nzito na likolee kwelikweli na hata mume au mpenzi wako anapokuja kula basi asiione lina matatizo au jepesi, mfanye awe analitamani kila siku kwani usipofanya hivyo na wenzako nje wakamtengenezea na akakosea kulila, ndiyo mwanzo wa kuhama kwenye jiko lako.
Uzuri wa mwanamke siyo sura tu bali hata katika mapishi kwenye jiko lenye kiwanja cha sita kwa sita. Ukiwa jikoni humo jitahidi kupika mboga, ukiamini kwamba ukitia tui, mumeo au mchumba wako hatabanduka na kwenda kutafuta chakula sehemu nyingine. Tumewahi kushuhudia wanawake wengi wakilalamika kuchukuliwa kwa waume wao au wapenzi wao au wachumba wao na wanawake wengine kisa ni jinsi wanavyowatayarishia tui na kila wakila wanaona ni hovyo tu.
Ubaya ni kwamba siku hizi wasichana wengi hawafundwi kama zamani ambapo walikuwa wakikusanyika wanawake watu wazima na kuwafundisha wasichana jinsi ya kutengeneza tui zito litakalomfanya mume asihangaike na mboga za nje.
Siku hizi wasichana wanaona mambo hayo kuwa ni ya kizamani na wala hawana haja ya kufuatilia kwa wanawake waliowapita umri ambao wameona mengi, hivyo kubaki kuharibu tui na kutotamanika. Ukiwa wa bush kwenye miti mikavu na vichaka unaachwa, sasa kwa nini usijifunze hata kwa kuibia kwa wenzako?
Shoga, acha nikupe kaubuyu kadogo! Wenzako wakipewa jembe kabla hawajaingia shambani wanaangalia kwanza kama wataweza kulilimia, halijaharibika!
Wanalichukuwa na kuingia shambani, wakimaliza kulima wanachukuwa nazi na kuanza kukuna, wanahakikisha wanapata machicha ya kutosha, wanakamua hadi tui lile zito walione likitoka! Wakionja huo utamu wake, mwanaume hatoki! Kwanza akafuate nini huko nje?
Uzuri wa siku hizi tui la nazi hata ukilila kwa chakula cha usiku tamu, chakula cha mchana tamu. Ukilila kipindi cha baridi tamu, kipindi cha joto tamu. Ukilila kwa kufunika chakula tamu, ukikifunua napo tamu.
Ukilila kwa kuimba nyimbo zote tamu, iwe Mchiriku au Taarab linakuwa tamu.
Shoga najua umenipata, basi yafanyie kazi niliyokuambia ili ndoa yako idumu.
Kwa leo sina mengi tuonane wiki ijayo! Kwa ushauri, nitumie meseji tu kwa namba yangu hapo juu nitajibu
No comments:
Post a Comment