Trending News>>

Mo awaita Wafaransa kuwekeza Tanzania

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL), Mohammed Dewji (Mo) amewaalika wawekezaji kutoka Ufaransa kuja kuwekeza Afrika Mashariki, hasa Tanzania.

Mo alitoa wito huo jana alipohudhuria tuzo za wawekezaji bora zilizoandaliwa na Chama cha Waajiri Ufaransa (Medef) kwa kushirikiana na taasisi ya Choiseul kuwatambua watu wenye mchango mkubwa kwenye jamii inayowazunguka.

Akiwa mshindi wa nafasi ya mjasiriamali bora Afrika, kipengele kipya kilichoongezwa mwaka huu, Mo aliitangaza Tanzania na kuwataka waandaaji kuzingatia nchi za Afrika zisizozungumza Kifaransa ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kwenye tuzo hizo.

“Tanzania ina fursa nyingi zinazohitaji uwekezaji. Kuna amani ya kutosha inayohakikisha usalama wa miradi ya kila mwekezaji. Uchumi wetu unakua kwa kasi kubwa ikilinganishwa na mataifa mengine,” alisema Mo.

Akiinadi Tanzania, alieleza msimamo wa Serikali na hasa vita inayoongozwa na Rais John Magufuli ya kupambana na rushwa, kuondoa urasimu na mpango wa kubana matumizi kwa kuondoa gharama zisizo za lazima.

“Serikali ya Tanzania ni ya kupigiwa mfano kwa uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma, isiyovumilia ubabaishaji,” alisema akiwataka wafanyabiashara waliohudhuria tuzo hizo kushirikiana na Afrika kukuza uchumi.

Medef, chama kikubwa zaidi cha waajiri nchini Ufaransa kina wanachama wenye miradi duniani kote kama vile Total, BNP Paribas, AXA Group na Micheln kimekuwa kikitoa tuzo za umahiri kwenye biashara na uwekezaji tangu 1988.

Licha ya tuzo ya Medef, mfanyabiashara huyo ameshashinda mara tatu, tuzo ya Taasisi ya Choiseul ya nchini humo; mwaka huu akiwa kijana chini ya miaka 40 mwenye ushawishi kiuchumi, huku akishikilia tuzo ya ‘Africa Person Of the Year 2015’ inayotolewa na Jarida la Forbes.

Mo aliielekeza tuzo hiyo kwa vijana wa Afrika ambao alisema ni nguzo ya maendeleo yanayotokea barani hapa na kuwataka wasikate tamaa kwa kila linalowakabili kwenye harakati zao za maisha na utafutaji. Pia, aliwataka kuwa wabunifu na kutumia vipaji walivyonavyo kujiletea maendeleo kwa kuchagua fursa zinazowazunguka popote walipo.

Akieleza matarajio yake kwa Afrika, alisema: “Maendeleo endelevu yanayojumuisha sekta binafsi yana umuhimu wa pekee. Ili kufanikisha hili, maskini ni lazima washirikishwe kama wazalishaji, waajiriwa na wateja wa bidhaa za miradi mikubwa.”

No comments:

Powered by Blogger.