Mh MAGUFULI KUONGOZA KIKAO CHA NEC LEO DESEMBA 13
Magufuli kuongoza kikao cha NEC leo
KIKAO cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakutana leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni kikao cha kwanza kuongozwa na Rais John Magufuli tangu achaguliwe kukiongoza chama hicho tawala Julai mwaka huu.
Juzi, Rais Magufuli aliongoza kikao cha Kamati Kuu ambacho kilipaswa kuwa cha siku mbili, lakini kikamaliza kazi zake juzi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari juzi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu kwamba mapendekezo au hoja zote zilizoibuliwa na wajumbe katika kikao hicho zitawasilishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kitafanyika jijini Dar es Salaam.
Nape hakueleza hoja na mapendekezo hayo yanayopelekwa NEC, lakini kwa ujumla kikao hicho ndicho chenye uamuzi wa kubariki mapendekezo yanayotoka katika kikao cha Kamati Kuu hivyo inatarajiwa kuwa itafanya maamuzi mbalimbali.
Miongoni mwa hayo ni uteuzi wa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Dimani Zanzibar, lakini pia huenda NEC ikabariki uteuzi wa wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho kama yatawasilishwa kwao na Mwenyekiti kutokana na nafasi mbalimbali kuwa wazi.
Naibu Katibu Mkuu Bara, Rajab Luhavi na aliyekuwa Kaimu Katibu wa NEC wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk Pindi Chana hivi karibuni wameteuliwa kuwa mabalozi wakati Nape pia anashikilia wadhifa wa uwaziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Aidha, aliyekuwa Msemaji wa chama, Christopher ole Sendeka mwishoni mwa wiki aliteuliwa na kuapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, hali inayoashiria kuwa mabadiliko katika Sekretarieti hayaepukiki.
Aidha, Nape aliwaambia waandishi juzi kuwa ajenda kuu katika kikao hicho cha Kamati Kuu ilikuwa ni tathimini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Alisema tathimini hiyo ilikuwa ni pana na imefanyika kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja ambayo ilifanyika kwa ngazi ya mikoa, wilaya na kata na wamemaliza tathimini na kuipeleka makao makuu ya chama ili kupitiwa na vikao vya maandalizi vya sekretarieti na vikao vingine kisha ikawasilishwa kamati kuu kwa ajili ya kujadiliwa.
Alisema baada ya tathimini hiyo kujadiliwa Kamati Kuu itapelekwa katika kikao cha Halmashauri Kuu leo ambacho ndio chenye maamuzi na kitapitia na kuangalia endapo kuna mambo yaliyopendekezwa na hatua za kuchukua kama mabadiliko na vitu vingine.
“Huu ni utaratibu wa kawaida katika chama chetu kila uchaguzi huwa inafanyika tathimini ambazo hutusaidia sana, kujua wapi tulifanya vizuri na wapi hatukufanya vizuri na mengineyo yote yaliyokuwa sehemu ya ushiriki wa chama katika Uchaguzi Mkuu, na tumekuwa tukifanya hivi katika chaguzi zote hali ambayo imeifanya CCM kuimarika zaidi,” alieleza Nape.
No comments:
Post a Comment