Maneno ya Juma Abdul baada ya Twite kuondoka
Beki nyota wa Yanga, Juma Abdul, amesema ni vigumu kusahau mchango wa kiraka Mbuyu Twite ambaye ametupiwa virago ili kumpisha Mzambia, Justine Zulu, kwani alikuwa ni zaidi ya mchezaji kikosini mwao.
Rasmi Twite ameondolewa kwenye kikosi huku Zulu maarufu kama Mkata Umeme akianza kuitumikia timu, lakini Juma Abdul anaamini Twite alikuwa injini ya mafanikio kwa kipindi alichokaa Jangwani kutokana na umahiri wa kucheza zaidi ya namba moja, jambo ambalo liliisaidia Yanga kwa sehemu kubwa.
Ikumbukwe Mnyarwanda huyo mwenye asili ya DR Congo, alihimili kucheza namba zote kwenye safu ya ulinzi, kiungo mkabaji ama kuchezesha timu, hivyo kuwa hazina kubwa ya Yanga.
Akizungumza jijini Dar es Salaam beki huyo wa zamani wa Mtibwa, alisema: “Twite kiukweli tutamkumbuka kwa mengi, pamoja na maelewano uwanjani, lakini uwezo wake wa kucheza karibu kila namba uliisaidia sana timu.
"Hakika huwezi kuzungumzia mazuri ya Yanga kwa kipindi alichokuwepo bila kumtaja alikuwa akiiokoa timu mara kadhaa wakati anapokosekana mchezaji yeyote hata mimi.”
Source: Championi
No comments:
Post a Comment