Mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Kampasi ya Dodoma yafana
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dokta Philip Mpango, amewataka wataalamu wa Mipango na Maendeleo Vijijini kufanyakazi zao kwa weledi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na ufisadi ili kuwawezesha wananchi hususan waishio vijijini kunufaika na huduma yao ili kujikwamua kiuchumi na kuodokana na umasikini
Dokta Mpango ametoa rai hiyo wakati wa mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilichoko eneo la MIYUJI mkoani Dodoma, ambapo wahitimu 1,641 wakiwemo wanaume 796 na wanawake 845 wametunukiwa tuzo zao katika kozi 11 zinazohusu Mipango, Maendeleo, Fedha na uwekezaji.
Amesema kuwa ubunifu na upangaji mzuri wa mipango ya maendeleo vijijini utaharakisha nia ya serikali ya kuwaondolea wananchi wake umasikini hivyo kuboresha maisha yao
Waziri huyo wa Fedha na Mipango, amewahimiza wahitimu hao kuja na mawazo mapya au njia mbadala za kukabiliana na changamoto za kukuza shughuli za biashara vijijini, hasa ukosefu wa mikopo na mitaji, bima, mfumo dume pamoja na mfumo duni wa uzalishaji na ukosefu wa masoko.
“Ninawaasa wahitimu wetu muwe wazalendo na mfanyekazi kwa bidii kokote mtakako kwenda ili muwe kioo cha chuo hiki kwasababu Tanzania yetu inawataka muwe wabunifu na kukataa kujihusisha na mambo yanayohatarisha amani, usalama na umoja wetu kama watanzania” aliongeza Dkt. Mpango
Aidha, amevishauri vyombo vya habari nchini kuandika habari za changamoto na fursa zinazowakabili wananchi vijijini badala ya kuandika na kutangaza mambo yanayodhalilisha nchi yao kwa kukosekana uzalendo
“Tumeshuhudia mafanikio makubwa waliyoyapata wakulima kutoka Wilayani Mbulu mkoani Manyara, na Njombe mkoani Iringa ambao wameongeza uzalishaji wa mazao yao ya vitunguu saumu, mahindi na maharagwe pamoja na kuongeza thamani ya mazao hayo, hizo ni habari nzuri za kuandika” alisisitiza
Kwa Upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini, Dkt. Frank Hawassi, amesema kuwa wahitimu wa chuo hicho wameandaliwa katika mfumo unaolenga weledi na umahiri utakao wawezesha kutekeleza majukumu yao kwa tija zaidi katika maeneo yao ya kazi.
Amesema kuwa wahitimu hao wameiva na wako tayari kuisaidia nchi kupiga hatua kubwa kimaendeleo katika kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Razack Lokina, ameiomba serikali kukisaidia chuo hicho kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa jengo la utawala, hosteli na upungufu wa wahadhiri ili kukiwezesha chuo hicho kuendelea kutoa elimu bora kwa wahitimu wake.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mwanafunzi bora wa shahada ya uzamili, Bi. Gemma Mafwolo, amesema kuwa wahitimu wa chuo hicho wameiva na wako tayari kutumika mahali popote hapa nchini kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya wananchi vijijini.
“Tunapenda kukuahidi kuwa tutatumia elimu tuliyoipata kwa manufaa mapana ya taifa letu kwa kuibua, kupanga, kutekeleza, kusimamia, kufuatilia na kufanya tathimini ya mipango na maendeleo katika nyanja zote za maendeleo” alisisitiza Mafwolo
Vilevile ameishukuru serikali kwa kuahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazokikabili chuo hicho ikiwemo ukosefu wa sehemu za malazi ya wanafunzi, maeneo ya michezo pamoja na upungufu wa wahadhiri.
Zaidi ya wataalamu wa mipango ya maendeleo vijijini 14,583, wamehitimu mafunzo yao tangu chuo hicho cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kianzishwe mwaka 1980 kikisimamiwa na Wizara ya Fedha na Mkipango.
Katika tukio jingine, waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amezindua jengo la pili la taaluma la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini lililojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 10.3 lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,250 wanaofundishwa kwa wakati mmoja.
Jingo hilo la ghorofa 7 lina kumbi 4 za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua watu 320 kila mmoja, madarasa 6 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kila moja, chumba kimoja cha maabara ya kompyuta chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 150 kwa wakati mmoja, ukumbi 1 wa mikuta (80), Stoo 2, kantini 1 na vyumba vya ofisi 32.
Mwisho
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (Wa pili kulia), akipata maelezo ya Chuo Cha Maendeleo ya Mipango Vijijini Kampasi Kuu ya Dodoma, kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Frank Hawassi (Wa pili kushoto) kabla ya kuanza kwa sherehe ya Mahafali ya 30 ya Chuo hicho kilichoko eneo la Miyuji, mkoani Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (wa pili kulia) akingalia moja ya machapisho yanayotolewa na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini wakati wa maonesho ya bidhaa na huduma zinazotolewa na chuo hicho wakati wa Mahafali ya 30 ya kampasi Kuu ya Dodoma. Anayetoa maelezo Kushoto ni Mkuu wa mradi wa Agra Dkt. Mark Msaki ambaye ni mhadhiri wa chuo hicho.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akiangalia viatu vya ngozi vilivyotengenezwa na mjasiliamali mdogo Bw. Stephano Chifwaguzi (nayeonesha bidhaa ya ngozi kiunoni) baada ya kuwezeshwa kiutaalamu na Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya, wakati wa mahafali ya 30 ya Chuo hicho Kampasi Kuu ya Dodoma.
Mhadhiri wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini, Ezekiel Kanile (kushoto) akimweleza waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa pili kulia) namna chuo hicho kinavyosaidia wakulima wa Vitunguu Saumu wilayani Mbulu Mkoani Manyara, wakati wa maonesho ya Bidhaa na huduma katika Mahafali ya 30 ya Chuo hicho kampasi Kuu ya Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akiongea na mkulima wa vitunguu saumu Bw. Boniface John, kutoka Wilayani Mbulu mkoani Manyara (aliyeshika kipaza sauti) wakati akielezea namna alivyofanikiwa kuongeza thamani ya zao hilo kwa msaada wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Dodoma wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika eneo la Miyuji, mkoani Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Jengo la pili la Taaluma lenye ghorofa 7 la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kampasi Kuu ya Dodoma, lililogharimu shilingi Bilioni 10.3. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Razack Lokina na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Dkt. Frank Hawassi wakifurahi kwa pamoja mara baada ya uzinduzi huo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akimpongeza Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Dkt. Frank Hawassi, kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Jengo la Taaluma la Chuo hicho lenye urefu wa ghorofa 7, lilojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 10.3 zilizotolewa na Serikali, baada ya waziri huyo kulizindua rasmi jengo hilo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) (katikati) akiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Prof. Razack Lokina (Kushoto) na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Frank Hawassi akiwa wameketi kwe moja ya kumbi za mihadhara iliyoko katika Jengo la Pili JIpya la Taaluma lililozinduliwa wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo hicho Kampasi Kuu ya Dodoma.
Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 30 ya Chuo cha MIpango ya Maendeleo Vijijini, Kampasi Kuu ya Dodoma, Mhe. Dkt Philip Mpango (Mb) pamoja na wahitimu wakiingia kwenye ukumbi wa J.K Nyerere uliopo Chuoni hapo kwaajili ya Mahafali ya 30 ya Chuo hicho ambapo wahitimu 1,641, wametunukiwa tuzo mbalimbali ngazi ya Astashada, Stashahada na Shahada.
Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akifurahia mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, yaliyofanyika Kampasi Kuu ya Dodoma katika eneo la Miyuji-mkoani humo.
Wajumbe wa Baraza la kumi na la tisa la uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Kampasi ya Dodoma, iliyoko katika eneo la Miyuji, mkoani humo.
Wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini pamoja na wageni waalikwa, wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika eneo la Miyuji, mkoani Dodoma
Wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini pamoja na wageni waalikwa, wawakiwa wamekaa kwenye ukumbi wa J.K Nyerere uliopo katika Chuo hicho Kampasi Kuu ya Dodoma wakisubiri kutunukiwa tuzo ama vyeti vyao wakati wa Mahafali ya 30 ya Chuo hicho yaliyofanyika katika eneo la Miyuji, mkoani Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (katikati) akiwatunuku wanafunzi wa Astashahada na Stashahada (hawamo pichani) tuzo zao katika kozi kumi na moja katika mahafali ya 30 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini- Dodoma yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu J.K. Nyerere – Miyungi Dodoma. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Razack Lokina na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Frank Hawassi.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (katikati) akimtunuku shahada mmoja wa wanafunzi
Meza Kuu ikiongozwa na waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya wahitimu wa Shahada baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwatunuku tuzo mbalimbali wahitimu wa Mahafali ya 20 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya Dodoma katika eneo la Miyuji mkoani humo
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akishukuru kwa Tuzo aliyopewa na uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa kutambua mchango wake wa kumsaidia Rais wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwaletea wananchi Maendeleo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Razack Lokina, ikiwa ni alama ya kutambua mchango wake katika kuwatumikia wananchi na kumsaidia Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutekeleza ahadi zake za kuwatumikia watanzania.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Fedha na Mipango)
No comments:
Post a Comment