Machinga noma wafunga mitaa Dar, maduka yahamia barabarani
HALI si shwari. Ndivyo tunavyoweza kusema baada ya baadhi ya mitaa katika miji iliyopo makao makuu ya mikoa mbalimbali nchini kufurika wafanyabiashara ndogondogo, maarufu ‘wamachinga’.
Hiyo imetokea siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli kutoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kutowafukuza maeneo ya katikati ya miji wafanyabiashara hao.
Katika miji mikuu ya mikoa, jana wamachinga walionekana wakiendelea na maandalizi ya kujenga vibanda na wengine wakipanga bidhaa zao chini.
Mapema asubuhi jana Dar es Salaam, MTANZANIA lilishuhudia mitaa kadhaa ya Kariakoo tayari wafanyabiashara hao wameweka shehena kubwa za bidhaa, huku wakiendelea kuzitandaza pembezoni na hata katikati ya barabara bila kujali wapitanjia wengine, hususani wanaotumia vyombo vya moto.
Mitaa iliyosheheni wafanyabiashara hao ni Kongo, Nyamwezi, Swahili, Sikukuu, Narung’ombe na Mchikichi.
Baadhi ya wafanyabiashara wa maduka walionekana kuduwaa, huku wengine nao wakihaha kutafuta nafasi za kutandaza bidhaa zao nje.
Wamachinga wengine walipanga bidhaa zao katikati ya barabara na kuacha sehemu ya kupita tairi za gari. Hali iliyofanya bidhaa zao kuwa uvunguni mwa gari.
Mmoja wa wamachinga walioweka bidhaa katikati ya barabara, Mtaa wa Kongo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Robert, aliliambia MTANZANIA kuwa mtaa huo ndio wenye wateja wengi, hivyo wanalazimika kugombania nafasi za kupanga biashara zao.
Msemaji wa wamachinga wa Kariakoo, Masoud Issa, alisema wanamshukuru Rais Magufuli kwa kuwaruhusu kufanya biashara zao katikati ya miji.
“Tunamshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwani amekuwa mtu wa mfano kwa kuwakumbuka wamachinga, ambao kwa miaka mingi tumekuwa tukionekana watu wasio na thamani wala akili,” alisema Issa.
Hata hivyo, Issa alisema ruhusa hiyo ya rais inahitajika udhibiti kwa kuwa wapo wafanyabiashara wenye maduka, ambao wanatumia agizo la rais vibaya kwa kutoa bidhaa zao madukani na kuzitandaza barabarani ili wasilipe kodi.
“Kuna watu wanatafuta vijana wanatoa nje bidhaa zao madukani wanazimwaga barabarani, ambako wanajua hawatadaiwa risiri na hawatalipa kodi,” alisema Issa.
MAKONDA LAWAMANI
Kiongozi huyo wa wamachinga alimtupia lawama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwa alikuwa akirudisha nyuma juhudi za viongozi wa jiji hilo kupata mwafaka wa wamachinga.
Alisema tangu awali mapendekezo yao waliomba watengewe mitaa minne ya Kongo, Nyamwezi, Swahili na Sikukuu, huku wakiweka meza kwa mpangilio pembezoni mwa barabara na kuacha nafasi za watu kuingia madukani na kuweka mapipa ya taka.
“Katika mpango huo, pia tulisema tupo tayari tupewe mashine za kukusanya ushuru na kukagua risiti za wafanyabiashara ili Serikali ipate mapato yake, lakini RC Makonda alipinga mapendekezo hayo na kuyavuruga,” alisema.
SOKO LA ILALA
Katibu wa Ulinzi na Usalama Soko la Ilala, Yahya Makuani, alisema Rais Magufuli yuko sahihi, lakini kitu cha kuzingatia katika barabara za pembeni za waenda kwa miguu zisiguswe kwa sababu usumbufu utakuwa mkubwa.
“Kuna mitaa kama Kongo, Muhonda, Sikukuu na Mkunguni wapewe wamachinga, ifungwe wafanye biashara.
“Lakini wakiruhusiwa kufanya biashara pia wawajibike kulipa tozo ndogo ndogo kama tunavyolipa sokoni, sisi wanalipa Sh 500 kwa siku kila mfanyabiashara, hiyo inasaidia usafi na kuimarisha ulinzi, inaenda halmashauri,”alisema Yahya.
SIMU 2000
Wafanyabiashara wengi waliohamishiwa katika soko lililopo Kituo cha Mabasi Sinza (Simu 2000), wamerejea barabarani baada ya agizo hilo la Rais Magufuli juzi.
Awali walikuwa wakifanya biashara eneo la Ubungo kabla ya kuhamishiwa hapo na aliyekuwa Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob.
Wafanyabiashara hao waliondoka mapema jana na kurudi barabarani kuanzia njiapanda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi Ubungo Mataa.
Akizungumza na MTANZANIA, Meneja wa soko hilo, Elichilia Hamis, alisema wafanyabiashara hao walianza kuondoka mapema asubuhi jana kurudi katika maeneo ya barabarani.
“Wengi wameondoka na kurudi barabarani, ambako awali waliondolewa na meya, vizimba vingi vimebaki wazi, katika baraza F, B na D ni kweupe kabisa, baraza E na C wamepungua mno na wale wakina mama waliokuwa wakiuza chakula wote wameondoka kabisa,” alisema.
Alisema katika soko hilo walikuwa na uwezo wa kukusanya mapato hadi Sh milioni nane kwa mwezi, lakini kwa hali ilivyo sasa mapato yanaweza kupungua,” alisema Hamis.
BUKOBA
Katika mji wa Bukoba wafanyabiashara ndogondogo wameingia kwa kasi eneo la katikati ya mji karibu na Hospitali ya Rufaa.
Wafanyabishara hao ambao wengi walikuwa wamehamishiwa maeneo ya pembezoni mwa mji, waliiambia MTANZANIA kuwa wamepokea kwa furaha agizo la rais la kuwarudisha mjini, ambako kuna wateja wa kutosha kuendesha biashara zao.
Katibu wa Soko la wafanyabiashara ndogondogo, Juvenali Kevis, alisema kuwa uamuzi wa baadhi ya wamachinga kurudi katika maeneo yao ya awali ni kutokana na sehemu waliyokuwa wamepewa kudorora kibiashara.
DC ASHTUSHWA
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo, alisema uamuzi walioufanya wamachinga hao si mzuri kwani sehemu wanazofanyia biashara ni maeneo ya shule na hospitali ya rufaa ya mkoa, jambo ambalo linaweza kukwamisha mpangilio uliokuwa umewekwa awali.
MWANZA
Wamachinga na wafanyabiashara ambao huendesha mnada katika eneo la Kiloleni jijini Mwanza kila Jumatano, jana nusura wazichape, wanaripoti Masyenene Damian, Peter Fabian.
Ugomvi huo ulitokea baada ya wafanyabiashara wa mnada kuwasili katika eneo hilo na kukuta wamachinga waking’oa meza zao na nyingine kuvunjwa kwa kisingizio cha kurudi mjini.
MACHINGA WAANZA UJENZI
MTANZANIA ilishuhudia wamachinga wakiendelea na ujenzi wa meza na mabanda ya biashara katika mitaa ya Makoroboi na Stendi ya Tanganyika.
Mbali na ujenzi wa mabanda, wengine waliendelea kuweka meza katika maeneo ya kandokando mwa barabara mbalimbali jijini humo.
SHIUMA WATOA KAULI
Katibu Msaidizi wa Shirika la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA), Yohana Chacha, alisema wamelipokea kwa mikono miwili tamko la Rais Magufuli kwakuwa limezingatia mahitaji yao.
Alisema hatua za Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na Ilemela ya kuwaondoa mjini iliwapunguzia morali wa kujitafutia riziki yao ya kila siku.
“Kauli ya rais imekosha nyoyo za wajasiriamali wa jiji la Mwanza, anavyosema tuvumiliane anatambua hali ya kipato cha Watanzania kwamba wanatafuta kwa shida, hasa ukizingatia Desemba ni mwezi wa sikukuu na sherehe mbalimbali na Januari tunakuwa bize kulipia kodi za mapango ada za shule,” alisema.
DANADANA ZA KISIASA
Baadhi ya wamachinga wametafsiri kauli na uamuzi huo wa Rais Magufuli kuwa ni danadana za kisiasa zenye lengo la kutuliza hasira za wamachinga na kujijenga kisiasa, huku akiharibu ari na morali ya utendaji kwa watendaji wake wa chini.
Mmoja wa machinga waliozungumza na MTANZANIA jana, eneo la Stendi ya basi ya Tanganyika, Samweli Vicent, alisema kauli ya rais ni ya kisiasa kwa kuwa wameruhusiwa kwa muda tu na bado hawajajua mwafaka wao wa uhakika licha ya kurudishwa katikati ya mji.
“Kurudi mjini rais anataka tu kutufurahisha na kutuliza hasira za wamachinga kwa kuwa tumesikia atafanya ziara ya kikazi Mwanza hivi karibuni, mtaona baada ya hapo itakuwaje,” alieleza Vicent.
ATAKIWA KUREJESHA FEDHA
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, James Bwire (CCM), alimtaka Mkurugenzi, Kiomoni Kibamba kurejesha Sh milioni 60 zilizokuwa zimeidhinishwa kuboresha miundombinu katika maeneo waliyotakiwa kuhamia wamachinga kwa sababu hazikufanya kazi.
Maeneo yaliyotakiwa kuboreshwa ni ya Mirongo, Sinai, Nyegezi, Igoma, Buhongwa na Mchafukoga- Igogo.
IRINGA
Baada ya Rais Magufuli kutaka wamachinga wasibughudhiwe, wafanyabiashara hao mkoani Iringa wamelipuka kwa shangwe, anaripoti Raymond Minja
Akizungumza na MTANZANIA jana mmoja wa wafanyabiashara wanaouza kwa kutembeza mikanda, viatu na soksi katika Stendi ndogo ya Miomboni mjini hapa, Michi Baraka, alisema kuwa kauli ya Rais ni ya kishujaa kwani walikuwa wakinyanyaswa kila kukicha na mgambo wa Manispaa ya Iringa.
Alisema kuwa uongozi wa manispaa ulikuwa ukiwataka kuhama maeneo wanayofanyia biashara na kuhamia katika soko la Ngome ambalo si rafiki kwa biashara.
“Huko nchi za wenzetu watu wanafunga mpaka barabara ili watu wapate angalau siku moja ya kufanya biashara, lakini hapa kwetu hiyo kitu kulikuwa hakuna,” alisema.
MOROGORO
Kauli ya Rais kuwarudisha wamachinga katikati ya miji, imezua sintofahamu kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Morogoro, anaripoti RAMADHANI LIBENANGA.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina gazetini, walisema kuwaruhusu wafanyabiashara hao kuendelea kufanya biashara zao popote, kutakwamisha mipango ya baadhi ya miji kupanda hadhi na kuwa majiji.
“Angalia siku moja tu tangu Rais atoe kauli hiyo, tayari barabara zote zimejaa na kufungwa, hatujui baada ya mwezi kama zitapitika kwa matumizi mengine,” alisema.
Mkazi mwingine wa Morogoro alisema kuwaruhusu machinga kufanya biashara popote, kutaumiza wafanyabiashara wakubwa ambao wanalipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Machinga wanapanga biashara nje ya maduka yetu, na siku zote wanauza vitu vyao kwa bei nafuu kwa kuwa hawalipi kodi, lakini sisi tunalipa kodi TRA,” alisema Kirian Mushi ambaye ni mfanyabiashara.
ARUSHA
Baadhi ya wamachinga katika Jiji la Arusha, wamepongeza uamuzi wa Rais Magufuli wa kuwaruhusu kufanya biashara maeneo mbalimbali bila kubughudhiwa na uongozi wa jiji.
Akizungumza na MTANZANIA mmoja wa wamachinga hao, Gedion Alfayo, alisema kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na uongozi wa jiji, huku wengine wakinyang’anywa bidhaa zao kutokana na kutokuwa na eneo maalumu la kufanyia biashara yao.
No comments:
Post a Comment