Trending News>>

LUKUVI AAGIZA VIONGOZI KUSIKILIZA KERO ZA ARDHI ZA WANANCHI NA KUZITATUA


Na Hassan Mabuye (Kitengo cha Mawasiliano - Wizara ya Ardhi)
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amekutana wakazi wa Shinyanga na kusikiliza kero zao za ardhi na kuzitatua ambapo wananchi walijitoka kwa wingi katika viwanja vya Zimamoto Nguzo Nane mjini Shinyanga ambapo Waziri Lukuvi amepokea kero zaidi ya 200 za ardhi mkoani Shinyanga zinazodaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na maafisa ardhi,wenyeviti wa mitaa waliojikuta wakishindwa kujibu kero hizo mbele ya waziri huyo. 
Waziri Lukuvi alisema baada ya kupokea kero hizo ataunda kikosi maalum cha wataalam watakaoweka kambi mkoani Shinyanga kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na wataitwa mmoja mmoja kisha kujibiwa kwa maandishi. 
“Kama mmekaa na kero za ardhi tangu mwaka 2008 mpaka leo,naomba mniamini basi mimi kwa sababu Waziri ndiyo mwenye majibu ya mwisho kuhusu kero zenu,nilichobaini viongozi hawasikilizi kero za wananchi, kuna kero zingine hazikupaswa kuletwa kwangu mngemalizana huko huko”,alieleza Waziri Lukuvi. 
“Kama kuna maafisa ardhi wamekuwa sehemu ya migogoro ya ardhi lazima wawajibishwe,haiwezekani wananchi waichukie serikali kwa sababu ya watendaji wasio waaminifu,kiongozi atayebainika kuigombanisha serikali na wananchi tutaachana naye”,aliongeza Lukuvi. 
Waziri Lukuvi ametoa wito kwa wananchi wenye kero za ardhi wanapotoa ushahidi wawataje kwa majina watu wote waliohusika katika kukuza migogoro ya ardhi na kusababisha wananchi kunung’unika kwa kukosa haki zao ili waweze kuchukuliwa hatua. 
Kufuatia udhaifu huo aliwataka viongozi akiwemo Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kupanga muda wa kusikiliza kero za wananchi ili kupunguza kero za wananchi. 
Wakizungumza mbele ya waziri huyo,wananchi walisema baadhi ya watendaji wa serikali,wenyeviti wa mitaa na maafisa ardhi wamekuwa chanzo kikubwa cha migogoro kwa kuendekeza rushwa na kujuana.  
Mheshimiwa William Lukuvi akiwa wilani kishapu Mkoani Shinyanga ameendelea na ziara ya kusikiliza kero za wananchi kuhusu masuala ya ardhi na kuzitatua. 
Akizungumza katika viwanja vya Ushirika katika mji wa Mhunze wilayani Kishapu wenye kata 25,vijiji 117 na vitongoji 660 wakati akisikiliza kero za ardhi kutoka kwa mwananchi mmoja baada ya mwingine,Waziri Lukuvi alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imedhamiria kumaliza kero za ardhi. 
Ziara hiyo imekuwa na manufaa kwa wakazi wa Kishapu baada ya waziri huyo kuahidi kuanzisha baraza la ardhi katika wilaya hiyo hivi karibuni na wiki ijayo atateua mwenyekiti wa Baraza hilo ili kutatua kero za ardhi na kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo katika wilaya ya Shinyanga. 
Lukuvi aliwataka maafisa wa ardhi nchini kushirikiana na sekta binafsi kupanga miji na wao kubakia kuwa wasimamizi wa taratibu zote kwani serikali haina uwezo wa kuajiri maafisa ardhi na mipango miji wengi. 
Waziri Lukuvi pia amepiga marufuku vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wawekezaji wasio waaminifu waliopewa vibali vya kuchimba madini kuwahamisha wananchi katika maeneo ya uchimbaji bila kuwalipa fidia. 
“Kama umepewa kibali na serikali cha kuendeleza eneo flani la mgodi wale wananchi wa pale lazima waondoke lakini waondolewe kwa heshima, wapewe fidia inayofanana na thamani ya mali zao zilizopo eneo lenye mgodi siyo fidia ya kupunza wananchi kama kulikuwa kuna nyumba wajengee nyumba zingine nzuri ndio uwaamishe”,alisema Lukuvi.
  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akisalimiana na Maafisa wa Serikali mkoani Shinyanga mara baada ya kuwasili katika wilaya hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.
 Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wakiwa katika foleni ya kukabidhi malalamiko yao ya migogoro ya ardhi na bahasha za kero za ardhi kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ili atolee ufumbuzi.
  Bahasha zaidi ya mia mbili (200) za kero za migogoro ya ardhi zikiwa zimepokelewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ili aitatue.
 Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wakiandaa maelezo kuhusu matatizo wanayokumbana nayo katika umiliki wa ardhi mkoani Shinyanga ili Waziri wa Ardhi ayatatue.
 Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wakiwa eneo la mkutano wakisubiri zamu ya kueleza kero za ardhi kwa waziri.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akitatua mgogoro wa ardhi wa Bibi Safina Ibrahim mara baada ya kuleta vielelezo vyake.
 Msafara wa Waziri wa Ardhi, ukiwa umewasili katika jengo la Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga kwa ajili ya kukutana na wakuu wa idara hususani wa sekta ya ardhi wa Kishapu kabla ya kwenda katika mkutano wa kusikiliza kero za wananchi katika mji wa Mhunze.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimkabidhi vitabu vyenye muongozo namna ya kupanga miji sambamba na kitabu chenye majina 33 ya makampuni yaliyojitolea kushirikiana na serikali kupima ardhi.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akitatua mgogoro wa ardhi wa wananchi wa Kishapu waliokuwa wanagombea eneo la makazi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimhoji Mthamini wa wilaya ya Kishapu Reuben Lauwo (mwenye shati ya bluu) na Afisa Ardhi wa wilaya ya Kishapu Grace Pius (gauni la kitenge) kwanini hawakumlipa fidia bwana Daudi Amos (wa kwanza kushoto) kama inavyostahiki.

No comments:

Powered by Blogger.