Trending News>>

Kiama chaja: Uhakiki wa Vigogo Wenye Mali Nyingi za kufuru

Balaa jipya kwa vigogo wenye mali kufuru

SIKU moja baada ya Serikali kutangaza kuwa inaandaa uhakiki kabambe wa mali za viongozi wa umma takribani 500 nchini, imebainika kuwa operesheni ya sasa itakwenda mbali zaidi kwa kufichua pia mali zilizofichwa na wahusika kwa kuziandikisha majina yasiyokuwa yao.

Aidha, imefahamika vilevile kuwa operesheni hiyo itawaweka matatani watu wanaoonekana kuwa na utajiri kufuru ndani ya kipindi kifupi, lengo likiwa ni kufahamu kama hawatumiwi na baadhi ya vigogo kumiliki mali zilizopatikana kwa njia haramu kwa nia ya kukwepa mkono wa sheria.

Taarifa ya kuwapo kwa mkazo zaidi wa operesheni hiyo ya aina yake imeifikia Nipashe ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki, kuutangazia umma juu ya kuwapo kwa uhakiki wa mali za viongozi wa umma kwa nia ya kujua kile walichojaza katika fomu zao na uhalisia wake.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na madai kuwa Sekretatieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma haina nguvu ya kutosha kuwabana
viongozi wanaojilimbikizia mali kwa kutumia vibaya madaraka yao huku wakiziandikisha mali zao kwa majina yasiyokuwa yao.

Hata hivyo, kupitia operesheni ya sasa, chini ya utawala wa awamu ya tano uliotangaza vita isiyokoma dhidi ya vitendo vya ufisadi, yaelekea hakuna tena mwanya wa kuficha mali kwa njia hiyo ya kuziandikisha kwa majina bandia ya ndugu, jamaa na marafiki.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Waziri Kairuki alisema mamlaka mbalimbali za dola zinashirikiana kwa karibu kufanikisha uhakiki huo, ambao utahusisha mlinganisho wa taarifa zilizotolewa na viongozi dhidi ya ukweli wa mali zao.

"Bajeti kwa ajili ya uhakiki huo ipo. Mwaka huu tutahakiki mali za viongozi 500 tukianza na viongozi 120 katika awamu ya kwanza.

Tutahakiki mali za viongozi wa aina zote. Watakaobainika wametoa taarifa za uongo, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria," alisema Kairuki.

Alizitaja baadhi ya taasisi zinazoshirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanikisha uhakiki huo ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na pia taarifa kutoka kwa wananchi.

Ipo pia Wizara ya Sheria na Katiba, chini ya waziri wake, Dk. Harrison Mwakyembe, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila kiongozi anazingatia maadili ya uongozi wa umma.

Kairuki aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwafichua viongozi wanaomiliki mali kwa kificho, huku baadhi wakitumia majina ya ndugu na jamaa zao katika kuonyesha kuwa ndiyo wanaozimiliki.

“Pamoja na uhakiki huu kufanyika, tunaomba wananchi wajitokeze kwenda kukagua daftari lenye matamko ya mali na madeni ya viongozi wa umma ili kuweza kujua kiongozi yupi hasa amedanganya kuhusu mali zake,” alisema Kairuki na kuongeza:

"Wananchi ndiyo wanawajua zaidi… watatusaidia kujua kile alichokiandika katika tamko lake la kiapo, ndicho anachokimiliki au ameificha Sekreterieti."

UFAFANUZI WA KISHERIA

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alipotafutwa na Nipashe jijini kuzungumzia suala hilo jana, alisema: "Kudanganya kiapo ni kosa kisheria na unaweza kushtakiwa."

Alisema mtumishi wa umma anayetoa taarifa za uongo kwenye kiapo chake, anakiuka sheria na anashtakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Mwaka 1995.

Kwa kuzingatia maelekezo hayo, Nipashe ilifuatilia Sheria hiyo na kubaini kuwa kila kiongozi wa umma anabanwa ataje mali anazomiliki.

Kifungu 9(1) cha Sheria hiyo kinasema: "Kila kiongozi wa umma atatakiwa, isipokuwa tu kama Katiba au Sheria nyingine zilizoandikwa zitakapohitajika vinginevyo, kumpelekea Kamishna tamko la maandishi katika hati rasmi linaloorodhesha mali au rasilimali zake, au mume au watoto wenye umri usiozidi miaka 18 na ambao hawajaoa au kuolewa."

Aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Maadili, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, aliiambia Nipashe kwa simu ja kuwa utaratibu unaotumika endapo mtumishi wa Serikali akitoa taarifa za uongo kuhusu mali zake ni kumtaarifu kwa barua mhusika huyo ili azirekebishe.

Ikiwa mtumishi husika atashindwa kuzirekebisha, alisema Tume ya Maadili hufanya uchunguzi kwenye vyombo husika kama vile Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) na (TRA) ili kujua mali husika za mtumishi huyo.

Jaji Kaganda aliendelea kueleza kuwa endapo mtumishi husika akigundulika baada ya uchunguzi huo alitoa taarifa za uongo na kushindwa kuzirekebisha baada ya kupewa nafasi hiyo, atafikishwa katika Baraza la Maadili kwa kuwa ni kosa la jinai kutoa taarifa za uongo.

"Baraza la Maadili hufanya kazi na Jeshi la Polisi na Takukuru ambao huchukua hatua mara mtumishi anapokutwa na makosa," alisema Jaji Kaganda.

MALI KUFURU
Miongoni mwa mali zinazodaiwa kufichwa na viongozi wanaotumia nafasi zao kujilimbizia utajiri kufuru ni pamoja na nyumba za kifahari, magari ya bei mbaya, majengo ghali mijini yanayokodishwa kwa shughuli za biashara na ofisi, umiliki wa hisa kwenye kampuni mbalimbali, umiliki wa biashara kubwa kama za hoteli, vituo vya mafuta na magari makubwa ya mizigo, utitiri wa viwanja na mashamba makubwa.

“Kuna baadhi ya watu huonekana kuwa ni matajiri wakubwa mitaani lakini ukiwafuatilia utagundua kuwa wenye mali wanaohusishwa nazo siyo wao bali viongozi wasio waadilifu. Kadri nionavyo, itakuwa vigumu kwa watu wa aina hii kutobainika kupitia uhakiki huu wa mali halisi za viongozi,” mmoja wa maofisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (jina tunalihifadhi) aliiambia Nipashe jijini jana.

Alisema kuna 'vigogo' serikalini ambao wako kwenye idara na taasisi nyeti wanamiliki mali nyingi lakini wameziandikisha kwa majina ya ndugu na jamaa zao.

"Uongozi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma utaanza uhakiki mali zote muda wowote kuanzia sasa lakini kitengo cha uchunguzi kimetangulia na kimeshaanza kazi hiyo," alisema ofisa huyo.

Chanzo: Nipashe

No comments:

Powered by Blogger.