Trending News>>

Kesi mauaji ya watafiti kutajwa tena Desemba 29


KESI ya mauaji ya watafiti wa Kituo cha Utafiti cha Selian Arusha (SARI) inayowakabili wakazi 29 wa kijiji cha Iringa Mvumi Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, inatarajiwa kutajwa tena Desemba 29, mwaka huu kutokana na upelelezi wake kutokamilika.

Watu hao wanakabiliwa na mashitaka matatu ya mauaji ya watafiti watatu, Nicas Magazine, Theresia Nguma na Faraji Mafuru huku gari lao lenye namba za usajili STJ 9570 aina ya Toyota Hilux Double Cabin likichomwa moto.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Amos Kwanga, Mashaka Nyambi, Victoria Lungwa, Wilson Mabwai, Sarah Chimanga na Daud Mangwata.

Wengine ni Peter Fwezi, Adrian Sudai, Charles Lemanya Fredrick Sudai na Tibu Ng’ambi, Bruno Lebedu, Jonas Makwawa,Erasto Masaka, Juma Chitongo, Cesilia Mwalu, Dorca Mbehu, Edna Nuno, Grace Masaulwa na Juma Madeha.

Wengine ni Albert Chimanga, Sosteness Mseche, Julius Chimanga, David Chimanga, Lazaro Kwanga, Yoram Samamba, Edward Lungwa na Simon Samamba.

Awali ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Chivanenda Luwongo, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Dodoma, Joseph Fovo kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba Mosi, mwaka huu katika kijiji cha Iringa Mvumi.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza makosa ya mauaji na kesi hiyo ambayo upelelezi wake haujakamilika imepangwa kutajwa tena Desemba 29, mwaka huu.

Kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana washitakiwa watabaki rumande hadi upelelezi utakapokamilika na kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa na hatimaye kutolewa hukumu. Watafiti hao walivamiwa na wanakijiji wa Iringa Mvumi na kuwakatakata kwa mapanga pamoja na silaha za jadi kisha kuwachoma moto hadi kufa.

No comments:

Powered by Blogger.