KASHFA Nzito Jeshi la Polisi na GSM
NSATO Marijani, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi pamoja na vigogo wengine wa serikalini wanatuhumiwa kushindwa kumsaidia Mtanzania Abdulswamadu Zacharia Omary (36) anayedai kutendewa vitendo vya kikatili, anaandika Josephat Isango.
Ukatili huo ni pamoja na kudhulumiwa mali na wafanyabiashara Said Sadi na Ghalib Said Mohamed.
Akisimulia mkasa huo huku akilia, kijana huyo anadai kufanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo kutaka kunyongwa ndani ya chumba cha mahabusu kilichopo Kituo cha Polisi Oystebay, kitendo anachosema kiliratibiwa na jeshi hilo kuwasaidia wafanyabiashara hao kupoteza ushahidi lakini amekuwa akilalamika bila kusaidiwa.
“Nimekuwa nikitumiwa na baadhi ya vigogo wa polisi wanajidai kutaka kunisaidia lakini wakifika kwa huyu jamaa wanakaa kimya, polisi wanashirikiana na huyu aliyekuwa mmiliki wa Home Shoping Centre (HSC), kutesa watu, na mimi wanakataa kunilipa milioni zaidi ya 250, nilizofanyia kazi nikiwa kwao Yemen,” anasema Omary.
Akisimulia mkasa wa tukio, Omary anasema alipewa zabuni ya kujenga jengo la ghorofa 3 nchini Yemen bila kupewa mkataba, akakataa lakini alinyang’anywa hati zake za kusafiria na kuteswa kikatili hali iliyopelekea akubali.
“Nilisaidiwa na watu wa shirika la kimataifa la wahamaji (International Organisation for Migration) kurudi Tanzania, lakini tangu nimerejea nchini, hawa jamaa wa iliyokuwa Home Shoping Centre na GSM wana nguvu serikalini hadi ndani ya vituo vya polisi,” anasimulia.
Katika barua yake ambayo amewaandikia viongozi kadhaa wa taasisi za serikali ambayo MwanaHALISI online imeiona Omary amesema, viongozi hao wamewekwa kwenye mfuko na wafanyabiashara hao, kiasi cha kuifanya serikali idharaulike.
“Unasikia, hili suala linajulikana pote polisi, afande Marijani analipotezea kwa muda mrefu, nilielekezwa kwa afande wa Interpol anaitwa Ngonyani.
“Pia Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, (Takukuru) wanalifahamu lakini ndugu yangu kila aliyetaka kunisaidia huishia kukaa kimya, natamani sasa kumwona rais anisaidie,” anasisitiza.
Omary katika andishi lake ametaja hata viongozi wa dini ambao wamekuwa wakijipatia fedha kutokana na tatizo lake ambalo polisi wameshindwa kulifanyia kazi.
Ninatishwa, ninaambiwa hawawezi kufanywa lolote ndani ya nchi hii, wakisikia nimelalamika kwenye ofisi yeyote ya serikali hata polisi hunijibu “wewe unapolalamika unaenda kwao, sisi tunawaita wanakuja tulipo, unajihangaisha.”
Anadai tarehe 23 Julai 2015 alitekwa na Gharib Said Mohamed pamoja na Faisal kisha kupelekwa Masaki na kwamba, alipigwa na akawa hajitambua.
“Nilipojitambua nilijikuta Kituo cha Oysterbay nimefunguliwa mashtaka likiwemo la kumtukana rais, kutaka kulipua Ikulu, kukutwa na silala na niliwekwa rumande siku 46 bila kufikishwa mahakamani na namba ya jalada ilikuwa OB/IR/6365/2015, na OB/IR/11770/2015.
Nilipofikishwa mahakamani nilikuta mashtaka tofauti ambayo yalifutiliwa mbali na hakimu sababu hayakuwa ya kweli.
MwanaHALISI Online, limewasiliana na afande Lucy Ngonyani, aliyeshughulikia suala hilo na kukiri kuwa, analifahamu, yupo likizo na yeye sio msemaji wa jeshi hilo.
Alipoulizwa Nsato Marijani, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo alisema, “huyo kijana anapaswa afike ofisini kuniona, kama suala lake halijatekelezwa sio kuja huko kwa vyombo vya habari.”
Mtandao huu uliwatafuta watuhumiwa hao (Said Sadi na Gharib Sadi Mohamedi) kupitia simu zao za mkononi, pamoja na simu zao kuita kwa muda mrefu, hazikupokelewa.
Na hata walipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu zao, hawakujibu.
Chanzo:Mwanahalisionline
No comments:
Post a Comment