Trending News>>

JK afanya Mazungumzo na Mhe. Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, Jijini Maputo

Rais Mstaafu na Kamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Kugharamia Fursa ya  Elimu  Duniani  (UN Education Commission on Financing Global Education Opportunity) Desemba 8, 2016, alikutana na Rais wa Msumbiji,  Mheshimiwa Filipe Nyusi alipomtembelea jijini Maputo, Msumbiji.

Katika nafasi yake ya Mjumbe Maalum wa Kamisheni hiyo, Rais Mstaafu amemkabidhi  Rais Filipe Nyusi Ripoti ya Kamisheni hiyo yenye mapendekezo ya namna Dunia inavyoweza kukabili janga la Elimu kwa kuwekeza katika Mpango wa Kizazi cha Elimu (A Learning Generation). Mpango huo unalenga kuleta mapinduzi makubwa ya Elimu katika nchi zinazoendelea ndani ya Kizazi Kimoja  (miaka 30). Azma kuu ya Mpongo huo ni kuwezesha ifikapo mwaka 2040, watoto wote kote duniani wawe wanapata elimu iliyo sawa, na kwa kiwango cha ubora unaolingana dunia nzima.
Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi Mhe. Rais Filipe Nyusi ripoti ya Kamisheni ya UN ya Elimu jijini Maputo, Msumbiji.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa sasa, hali ya elimu katika nchi zinazoendelea inalingana na ile ambayo nchi zinazoendelea zilikuwapo miaka 70 iliyopita. Aidha, ripoti inasisitiza kuwa, ikiwa nchi zinazoendelea zitaendelea kwa kasi ya sasa, itazichukua nchi hizo kati ya miaka 90 na 110 kufikia viwango vya sasa vya nchi zilizoendelea. 

Aidha, ripoti inatahadharisha kuwa takribani ajira bilioni 2 zitakufa ifikapo mwaka 2050 kutokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo asilimia 70 ya kazi hizo ziko katika nchi zinazoendelea. Hivyo, nchi zinazoendelea zinapaswa kuangalia upya aina ya elimu na stadi zinazotolewa ili kuendana na wakati ujao.
Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akimpitisha Mhe. Rais Filipe Nyusi katika ripoti ya Kamisheni ya Elimu kuhusu Mapendekezo Mahsusi kwa nchi ya Msumbiji.

Kwa ajili hiyo, Kamisheni inapendekeza njia mpya na bora za kufanya mageuzi katika elimu ikiwemo kuongeza usimamizi, kupanua fursa, kuingiza ubinifu na teknolojia na kuongeza uwekezaji katika elimu kwa kushawishi ushiriki wa Jumuiya ya Kimataifa na Sekta Binafsi. Iwapo mapendekezo hayo yatatekelezwa, nchi zinazoendelea zinaweza kufidia pengo hilo ndani ya miaka 30 ijayo. Rais Mstaafu ameiomba Msumbiji kujiunga na Mpango huo.

Kwa upande wake, Rais Nyusi amepokea kwa furaha taarifa hiyo na kuelezea nia na dhamira ya nchi yake ya kujiunga na Mpango wa Kizazi cha Elimu. Kufuatia mazungumzo yao, mapema baadae  Rais Mstaafu alikutana na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Adriano Maleane, Naibu Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Elimu ya Fundi Mhe. Leda Hugo na Naibu Waziri wa Elimu Mhe. Armingo Ngunga kujadili mapendekezo mahsusi ya Kamisheni kwa nchi ya Msumbiji.
Rais Mstaafu na Mjumbe wa Kamisheni ya Elimu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Mhe. Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, jijini Maputo.

Ziara ya Rais Mstaafu itamfikisha katika nchi 14 barani Afrika ambapo zimechaguliwa katika awamu ya kwanza ya mpango huo. Tayari amekwishazitembelea nchi za Uganda, Malawi, Ethiopia na Msumbiji.na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa nchi hizo.
Mhe. Rais Mstaafu Jakaya Kikwete katika mkutano wake na Waziei wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri wa Elimu, Naibu Waziri wa Elimu ya Juu wa Serikali ya Msumbiji.
Rais Mstaafu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete katika picha ya pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri wa Elimu, Naibu Waziri wa Elimu ya Juu wa Msumbiji.

No comments:

Powered by Blogger.