Trending News>>

Don King, Mayweather waipa somo Tanzania


Promota wa masumbwi nchini, Juma Ndambile (kulia) akiwa na bondia wa Marekani, Floyd Mayweather. Chini, Ndambile akiwa na bondia wa zamani wa uzito wa juu wa Marekani, Evander Holyfield.

Dar es Salaam. Kongamano la Dunia la Masumbwi limeanza kuleta neema nchini baada ya promota maarufu duniani, Don King na bondia namba moja, Floyd Mayweather kujitosa kuhakikisha Tanzania inaandaa mapambano makubwa ya ngumi.

Hayo yalibanishwa na promota wa ngumi nchini na meneja wa bondia, Francis Cheka, Juma Ndambile aliyehudhuria Kongamano la Baraza la Ngumi la Dunia lililomalizika jana nchini Marekani.

Katika kongamano hilo la siku tatu, Ndambile alipata fursa ya kukutana na wadau mbalimbali wa ngumi duniani, wakiwamo mabondia Evander Holyfield, Wladimir Klitschko, Mayweather, Don King na Laila Ali, mtoto wa marehemu Muhammad Ali.

Ndambile alisema kongamano hilo limetoa funzo kwake kuhakikisha wanaandaa mapambano makubwa nchini.

“Niliongea na Don King na Mayweather wenye rekodi kubwa katika kuandaa na kucheza ngumi, kiukweli muongozo walionipa tukiufuata utaleta neema na kukuza ngumi zetu kimataifa.

“Wamenielimisha namna ya kuandaa ngumi, kuwasimamia mabondia, kupata udhamini na kunisisitiza ngumi ni moja ya michezo yenye fedha kama ikipata muongozo mzuri kwani una mashabiki wengi duniani,” alisema Ndambile na kuongeza:

“Don King alinieleza namna ya kupata udhamini hata kutoka nje ya nchi kwani kwa sasa dunia imegeuka kijiji, ukweli wenzetu wamepiga hatua, kongamano hili limenisaidia kuuelewa zaidi mchezo wa ngumi.

“Nitautumia uzoefu nilioupata kuendeleza ngumi hapa nchini, tumejenga urafiki na mabondia na mapromota wakubwa duniani, kwa baadaye tukienda vizuri naweza hata kuwaalika kuja kucheza au hata kushiriki au kusimamia mapambano nitakayokuwa nikiandaa.”

Katika hatua nyingine, Ndambile ameondoka jana Marekani na kwenda moja kwa moja India kumsapoti Cheka kwenye pambano lake la ubingwa wa mabara dhidi ya Mjerumani mwenye asili ya India, Vijenger Singh.

Cheka na Singh watazichapa Jumamosi hii pambano la uzani wa super middle kg 76 la WBF, kama atashinda atapanda kwenye viwango vya ubora vya dunia.

No comments:

Powered by Blogger.