UTAFITI: Wanawake vichaa ni wengi kuliko wanaume
Inadaiwa kuwa kwenye wanawake watano, mmoja anasumbuliwa na matatizo ya akili yanayotokana na msongo wa mawazo, wasiwasi na huzuni, ukilinganishwa na mwanamume mmoja kati ya wanane, utafiti umebaini.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Oxford, Daniel Freeman anasema wanaume wanaopata ugonjwa huo ni wale wanaoendekeza unywaji wa pombe na utumiaji wa dawa za kulevya.
Anasema idadi hiyo ya wanawake wanaosumbuliwa na maradhi ya akili kutokana na aina ya maisha wanayoishi yanayowasababishia wasiwasi, msongo wa mawazo na huzuni.
Mbali ya utafiti huo ambao ulichapishwa katika Jarida la Monitoring Psychology umeonyesha kuwa wanawake wana kabiliwa na matatizo ya akili kwa asilimia 40 zaidi ya wanaume kutokana na matatizo ya familia, mateso ya mapenzi, tamaduni na kulemewa na malezi.
Sababu nyingine inayowasababishia matatizo ni kufanya kazi za nyumbani kama walezi na watunza familia ikiwamo kuhakikisha inapata mlo wa siku.
Profesa Freeman anasema uchunguzi wa maradhi ya akili unaofanywa kila mwaka nchini Uingereza, umebaini wanawake wana matatizo ya saikolojia asilimia 20 zaidi ya wanaume.
Alisema miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha ongezeko hilo kwao ni kutokana na kuumizwa zaidi na maisha yawe ya ndoa, familia, mapenzi, jamii kuliko wanaume.
Anafafanua kuwa wanawake wanasumbuliwa na msongo wa mawazo na sonona mambo ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuchanganyikiwa na hatimaye kuwa na maradhi ya akili.
“Wanawake wanaishi na sonona kutokana na msukumo wa aina ya maisha wanayoishi, jamii zinazowazunguka na zinavyowachukulia ikiwamo kuhusishwa na kesi nyingi ikiwamo kujadili namna wanavyoendesha maisha yao na familia zao, tofauti na wanaume ambao hata wakiwa na matatizo kiasi gani hakuna anayejadili.
Alisema licha ya uchunguzi kuonyesha wanawake na wanaume wanatofautiana kupata maradhi ya akili, kutokana na tamaduni, lakini siyo ushahidi wa kuonyesha kuwa wanawake wengi wana tatizo hilo.
Anafafanua kuwa kwa kawaida wanawake wanasumbuliwa na matatizo zaidi ya wanaume ikiwamo wasiwasi, huzuni na kusumbuliwa na matatizo ya watu wengine kwenye familia.
“Kwa ujumla kwa maisha ya sasa katika familia, wanawake wapo katika hatari ya kupata maradhi ya akili zaidi kutokana na majukumu yao ya kila siku,” alisema Dk Freeman.
“Hivyo itakuwa ni makosa kwa kuainisha matatizo ya afya ya akili kuwa ni tatizo la wanawake. Viwango vya matatizo ya akili ni vikubwa kwa jinsi zote mbili, isipokuwa inatofautiana sababu na ndiyo maana upande mmoja unaonekana unaongoza.
Kwa mujibu wa Profesa Freeman watu 300 kati ya 1,000 hukabiliana na changamoto ya kuwa na matatizo ya afya ya akili kila mwaka.
Profesa alisema licha ya kutokuwapo kwa tofauti ya jinsi katika maradhi ya akili, wanawake wanapata matatizo hayo.
Bingwa wa tiba ya akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Cassian Nyandindi anasema sababu za wanawake kuathiriwa zaidi na maradhi ya akili hutokana na kusumbuliwa na maradhi ya sonona.
Anasema sababu za mtu kupata maradhi ya akili zipo nyingi, lakini inayoongoza ni sonona na wanawake wengi wanasumbuliwa na tatizo hilo, ndiyo maana inaonekana wao wanaongoza kuumwa maradhi hayo.
Anafafanua kuwa wanawake pia wanakabiliwa na mambo mengi ya kitamaduni ambayo huwalenga zaidi wao kuliko wanaume.
Akizungumzia tatizo hilo Tausi Muhsini anasema amewahi kushuhudia ndugu yake ambaye kwa sasa amefariki dunia alipata maradhi ya akili baada ya kumfumania mumewe.
“Alimfumania mumewe akiwa na ndugu yetu akachanganyikiwa hadi anafikwa na umauti miaka 10,” alisema Muhsini.
Utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la psychological Today la nchini Uingereza umeonyesha kuwa asilimia 10 ya wanawake huchanganyikiwa na kuugua maradhi ya akili baada ya kufanya jambo tofauti, ukilinganisha na asilimia nne tu ya wanaume ambao huwa hivyo.
Profesa aliyesimamia utafiti huo Aiken Ackerley alisema wanaume wanaopata matatizo hayo ni wale wanaojihusisha na matumizi ya pombe na dawa za kulevya kupitiliza.
Anasema tofauti ya wanawake na wanaume ni wanawake kujichanganya katika jamii kuliko wanaume ambao ni nadra kujichanganya kwenye jamii inayowazunguka na huwa na marafiki wanaofanya nao kazi.
“Wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa huu ni wengi kwa sababu za kisaikolojia kama vile huzuni, wasiwasi, matatizo ya kulala, matatizo ya ngono, na matatizo ya kula,” alisema Profesa Ackerley.
Alifafanua kuwa tafiti nyingi kuhusu suala hilo alizosimamia zilibaini kuwa asilimia tisa ya wanawake walishindwa kuvumilia huzuni huku asilimia tano ya wanaume wakichukulia kama jambo la kawaida. Alisema ni asilimia 23 ya wanawake wanasumbuliwa na ugonjwa wa wasiwasi ukilinganisha na asilimia 14 ya wanaume wanaosumbuliwa na ugonjwa huo.
Profesa aliyesimamia utafiti huo Aiken Ackerley alisema siyo kwamba wanawake wanasemwa vibaya katika hili, isipokuwa ni ukweli usiopingika kuwa wanawake wanakabiliwa na ugonjwa wa akili.
No comments:
Post a Comment