Trending News>>

Mawaziri kufuatilia ubadhirifu EPZA Bunda

MAWAZIRI watatu wameahidi kulivalia njuga suala la tuhuma za ubadhirifu wa fedha za fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yalichukuliwa na Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji wa Kiuchumi (EPZA), wilayani Bunda.

Mawaziri hao ni wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, ambaye atashirikiana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene.

Mwijage alitoa ahadi hiyo kwa niaba ya mawaziri wenzake na baada ya kuwauliza papo hapo kama wapo tayari, walikubali. Hatua hiyo ilitokana na swali la nyongeza la Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya (Chadema), aliyesema Waziri Mwijage, alidanganywa na wasaidizi wake waliomuandalia majibu ya swali lake la msingi kuhusu fedha ya fidia walizolipwa wananchi hao.

Bulaya alisema wananchi hao walilipwa Sh bilioni 1.240 lakini Mwijage katika majibu ya swali lake la msingi, alisema wamelipwa Sh bilioni 2.3. Katika swali la msingi, Bulaya alihoji ni lini wananchi wa vijiji vya Guta na Tairo, ambao ardhi yao ilichukuliwa takribani miaka saba iliyopita kwa ajili ya mradi wa EPZA italipwa?

Akijibu swali la msingi, Mwijage, alisema eneo lililoainishwa awali lenye hekta 2,200 likijumuisha vitongoji vitatu, lilipunguzwa na hivyo kubakiwa na eneo la Kitongoji cha Kirumi tu.

Alisema kwa mujibu wa uthamini, fidia iliyotakiwa kulipwa awali kwa ajili ya eneo lote ni Sh bilioni 3.477 lakini baada ya kupunguzwa, fidia iliyotakiwa kulipwa katika kipindi cha miezi sita bila riba ni Sh bilioni 2.143.

“EPZA ilipeleka Halmashauri jumla ya Sh bilioni 2.358 kwa ajili ya malipo ya fidia ikijumuisha riba kwa wananchi wote hao hata hivyo, Chacha M. Marwa, Gati M. Marwa na Juma W. Mgoba bado wanadai jumla ya Sh milioni 21.943,” alieleza Waziri.

Kutokana na ufafanuzi huo, Bulaya, alisema Mwijage alidanganywa kwani kiasi cha fedha kilichotumika kulipa fidia kwa wananchi hao ni Sh bilioni 1.240 pekee.

“Nasikitika kwamba mheshimiwa waziri umedanganywa, huyo mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wanaoshukiwa kuhusika na ubadhirifu huu walishatumbuliwa kwa sakata hili, ninachotaka kujua ni je, upo tayari kuagiza CAG, (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) na Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) kuchunguza waliokuwa wakilindwa na wakuu hao wawajibishwe?” Alihoji Bulaya.

No comments:

Powered by Blogger.