WATUMISHI WASIO WAJIBIKA WATAFUTE MLANGO WA KUTOKEA
WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge amewakemea Watumishi wa umma wasiowajibika na wanaofanya kazi kwa mazoea kuwa watafute mlango wa kutokea kwa kuwa wamekuwa chanzo cha kufa kwa miradi mingi ya serikali.
Pia waziri huyo alisema hakuna maji ya bure na kuwataka wananchi Ukerewe kuchangia gharama za huduma ya maji watakayoyatumia baada ya kukamilika kwa mradi wa Maji Nansio ili uwe endelevu na kuwawezesha watu wengine wa serikali na binafsi kupata huduma hiyo.
Mhandisi Lwenge alisema juzi mjini Nansio Ukerewe alipozungumza na baadhi ya wananchi, wadau na watumishi wa idara za Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo mara baada ya kukagua chanzo cha maji Nebuye na kituo cha huduma ya majitaka Hamkoko.
“Mradi huu wa Maji Nansio na kituo cha maji taka ambao umegharimu bilioni 13 ni mzuri ni wa pekee nchini.Wengine watakuja kujifunza hapa na utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 8 za maji kwa siku licha ya changamoto ya uhaba wa wahandisi wa ujenzi, umeme na mitambo,” alisema Mhandisi Lwenge.
Waziri huyo wa Maji alisema serikali imedhamiria kuwa ifikapo mwaka 2020 asilimia 100 ya wananchi wa Ukerewe wapate maji safi na salama kwa maeneo mengine asilimia 85 na hivyo kazi ya mazoea imepitwa na wakati.
“ Tunalo deni kwa waliotuchagua baada ya kuona ilani inatekelezeka.Kazi ya mazoea imepitwa na wakati,watumishi ambao hawatawajibika watafute mlango wa kutokea kwa sababu miradi mingi ya serikali inakufa kutokana na watendaji kutowajibika.Tuutunze miradi huu uwe endelevu,”alisema Lwenge.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akikagua mradi wa kituo cha kutibu maji taka kilichopo Hamkoko wilayani Ukerewe, mwenye fulana ya michirizi ni mhandisi mshauri wa mradi huo Mhandisi Edward Kazimoto na kushoto mwenye kofia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella.Nyuma kushoto kwa waziri ni Mkurugenzi wa MWAUWASA Mhandisi Anthony Sanga. Picha Na Baltazar Mashaka.
Mhandisi mshauri wa mradi wa Usafi wa Mazingira Ziwa Victoria (LVWATSAN) mhandisi Edward Kazimoto kitoa ufafanuzi wa ramani (michoro) ya miundo mbinu ya chanzo cha Maji Nebuye na kituo cha kutibu maji taka cha Hamkoko kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge (mbele) mwenye shati la mchanganyiko wa rangi.Kusjhoto mwenye suti ya rangi ya kahawia ni Mkurugenzi mtendaji wa Mwauwasa Mhandisi Anthony Sanga.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akiangalia mitambo ya kusukuma maji katika chanzo cha Maji Nebuye wilayani Ukerewe juzi.kushoto ni mhandisi mshauri wa mradi wa Usafi wa Mazingira Ziwa Victoria (LVWATSAN) mhandisi Edward Kazimoto. Na Baltazar Mashaka.
No comments:
Post a Comment