Trending News>>

Ujue ugonjwa wa kiharusi (stroke)


Kiharusi ni ugonjwa ambao huathiri ubongo na ufanyaji kazi wake. Hujulikana kama stroke au brain attack kwa Kiingereza. Unapopata kiharusi, seli za sehemu fulani za ubongo hushidwa kufanya kazi kutokana na damu kushindwa kufika kwenye seli hizo za ubongo. Kiharusi huweza kuathiri sehemu yoyote ya ubongo, na hivyo kuathiri ufanyaji wa shughuli za kila siku za mgonjwa.

Ugonjwa huu ni hatari na mara nyingi hujitokeza ghafla, ingawa wakati mwingine kuna dalili unazoweza kupata kuashiria ugonjwa huu. Dalili hutegemea na sehemu ya ubongo iliyoathirika. Sehemu kubwa ya ubongo ikiathirika huweza kusababisha mtu kushindwa kuongea, kujitambua na wengi hushindwa kurudi hali zao za kawaida.

Huu ni ugonjwa hatari ambao unaweza kusababisha mtu kupoteza maisha ghafla. Hivyo ni muhimu sana kuwahi hospitali kwa ajili ya matibabu. Pamoja na matibabu mazuri, kuna uwezekano mgonjwa akapata ulemavu wa maisha kutokana na kiharusi. Uwezekano wa kupata kiharusi huongezeka kadri umri unavyoenda.

NAMNA KIHARUSI KINAVYOTOKEA
Ili kufanya kazi zake, seli za kwenye ubongo hutegemea kupata virutubisho na oksijeni kutoka kwenye damu. Kukosa damu hata kwa dakika moja, huathiri kwa kiasi kikubwa uafanyaji kazi huu. Seli hizi zinaweza kufa kabisa kama zikikosa damu kwa dakika 5, na huwa haziwezi kutengeneza seli mpya.

Kwa hiyo pale inapotokea mshipa wa damu wa sehemu fulani ya ubongo umeziba au kupasuka, damu hushindwa kufika kwenye sehemu hiyo na hivyo seli zake zitashindwa kufanya kazi vizuri. Hali hii ikiendelea zaidi, seli hizo zitakufa kabisa. Kila sehemu ya ubongo huratibu kazi maalumu mwilini, mfano kuongea. Seli zinazoratibu kazi fulani zinapokufa, kazi hizo hushindwa kufanyika tena na hivyo dalili za kiharusi hujitokeza ikitegemea na sehemu ya ubongo iliyoathiirika.

KUNA AINA MBILI YA KIHARUSI:

  • Kiharusi kutokana na mishipa ya damu kuziba kwenye ubongo (ischemic stroke)
  • kiharusi kutokana na mishipa ya damu kupasuka kwenye ubongo (hemorrhagic stroke)

Mishipa ya damu kuziba kwenye ubongo (ischemic stroke) ni aina ya kiharusi kinachojitokeza zaidi kwa kiasi cha silimia 80, asilimia nyingine hutokana na mishipa ya damu kupasuka.

DALILI ZA KIHARUSI
Ugonjwa huu unaweza kujitokeza haraka na ghafla bila kutarajia. Na dalili hizi zinaweza kutokea kwenye sehemu yoyote ya mwili. Unapopata kiharusi unaweza kupata dalili zifuatazo:

  • Kushindwa kuongea au kuelewa. Unaweza kupatwa na hali ya kuchanganyikiwa, kushindwa kuongea ua kuelewa ghafla.
  • Kukosa nguvu au ganzi upande mmoja wa mwili. Ghafla tu unaweza kupatwa na hali ya kukosa nguvu, ganzi kwenye uso, mkono au mguu, hasa upande mmoja wa mwili. Mdomo kuelekea upande mmoja unapocheka, kushindwa kunyanyua mkono upande mmoja.
  • Kushindwa kuona vizuri. Hali ya kushindwa kuona vizuri inaweza kujitokeza ghafla. Inaweza kuwa kwa macho yote au jicho moja tu.
  • Kushindwa kutembea. Ghafla tu unaweza kushindwa kutembea kutokana na kupata kizunguzungu kikali, kukosa uwiano kwa ghafla.
  • Maumivu makali ya kichwa ghafla.
  • Dalili nyingine ambazo unaweza kupata ni kupoteza fahamu, degedege (convulsions), kushindwa kula, kushindwa kuzuia choo.

Kiharusi ni ugonjwa unaohitaji matibabu haraka sana. Kadri mgonjwa anapozidi kuchelewa kupata mtibabu ndivyo seli za ubongo zinavyozidi kufa. Kufa kwa seli hizi kutasababisha ulemavu kwa mgonjwa.

SABABU HATARISHI ZA KIHARUSI KUTOKEA
Vitu au tabia zifuatazo huongeza hatari ya kiharusi kutokea kwako:

  • Shinikizo la Damu La Kupanda
  • Uvutaji sigara
  • Magonjwa ya moyo
  • Magonjwa kama Kisukari
  • Kiwangi kikubwa cha lehemu kwenye damu
  • Kutofanya mazoezi
  • Uzito mkubwa
  • Unywaji wa pombe kiholela


VIPIMO
Unapopata tatizo hili unaweza kufanyiwa vipimo vifuatavyo ili kujua aina ya kiharusi ili upate matibabau sahihi.

Vipimo Vya Damu:

  • Complete Blood Count
  • Clotting factors
  • Kipimo cha CT Scan ya Ubongo
  • Kipimo cha MRI ya Ubongo


KUJIKINGA NA KIHARUSI
Kujikinga usipate kiharusi ni kitu muhimu sana, kwani hauwezi kujua kikitokea kitakuathiri namna gani. Kuna tabia hatarishi nyingi ambazo unaweza kuziondoa ka kufanya mabadiliko fulani katika maisha yako kama tutakavyoona hapo chini.


  • Acha kuvuta sigara
  • Shinikizo la damu la kupanda (hypertension). Fanya mazoezi, kula mlo kamili, dhibiti uzito,punguza chumvi na tumia dawa kudhibiti presha.
  • Kisukari.
  • Magonjwa ya moyo.
  • Fanya Mazoezi.
  • Dhibiti Uzito Wako.

No comments:

Powered by Blogger.