Trending News>>

Shahiri maalum kwa wanafunzi wa kidato cha 4

NAWAUSIA KIDATO CHA NNE

Leo kalamu nashika, kutoa yangu maoni,
Yasikize kwa hakika, kisha weka akilini,
Wakati umeshafika, wakuanza mtihani,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Wosia nauandika, kwako wewe ikhwani,
Machache nitatamka, yakufae darasani,
Ni vema ukayashika, usije yatupa chini,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Wahi mapema kufika, usichelewe shuleni,
Usijibu kwa haraka, bila swali kubaini,
Lisome na kuridhika, ujue lataka nini?
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Yasome maelekezo, kisha anza mtihani,
Tena fata muongozo, ulioandikwa ndani,
Tuliza yako mawazo, usome kwa umakini,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Usije ukachachawa, ukiona mtihani,
Ni vema ukishapewa, kwanza uuweke chini,
Uwaze na kuwazuwa, ondoa hofu moyoni,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Kumbuka kusoma swali, urudie maratani,
Usipuuzie hili, nakusihi ikhwani,
Kisha uanze na swali, lile lenye ahuweni,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Tena usigilizie, kwa mwenzio wa pembeni,
Wala usitizamie, kwa hilo kuwa makini,
Mwenyewe jisaidie, na kumuomba Manani,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Usije kukurupuka, ukamuiga fulani,
Ukafanya kwa haraka, ili utoke chumbani,
Utakuja kuanguka, na ufeli mtihani,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Pale utapomaliza, kuujibu mtihani,
Ujaribu kuangaza, kuhakiki kwa undani,
Swali ulilobakiza, usiliache hewani,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Kaditama ya utunzi, kalamu naweka chini,
Wosia kwa wanafunzi, wahitimu ushikeni,
Awaongoze mwenye enzi, mfaulu mtihani,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Mtunzi ni Ulamaa, nawambia kwaherini,
Msije kata tamaa, fanyeni kwa umakini,
Ni vema mvae saa, muelewe muda gani,
Ushike wangu wosia, ewe kidato cha nne.

Mtunzi: Ulamaa Hemed
0717 501557

No comments:

Powered by Blogger.