RAIS MAGUFULI LEO AMEKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA BIASHARA KUTOKA CHINA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 14 Oktoba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe.Qian Keming ambapo viongozi hao wamekubaliana kuharakisha miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili ukiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kati.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Rais Magufuli amemueleza Mhe. Qian Keming kuwa Serikali yake ya awamu ya tano inataka kuona mambo yakifanyika na kutoa matokeo bila kupoteza muda na kwamba angependa wadau wa maendeleo hasa nchi ya China ambayo ni ndugu na rafiki mkubwa wa Tanzania iende katika kasi hiyo hiyo.
Rais Magufuli ameuzungumzia mradi wa ujenzi wa reli ya kati ya kutoka Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na kuunganisha nchi za Rwanda na Burundi ambao Tanzania imetenga Shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi katika bajeti hii, kwa kutaka China ambayo imekubali kushiriki katika ujenzi iendane na kasi ya Serikali yake.
>>>Mhe. Qian Keming sisi tumeamua kuanza ujenzi na tayari Wakandarasi 32 wamejitokeza kuomba kujenga reli ya kati kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro umbali wa kilometa 200 za mwanzo na tutatumia fedha zetu wenyewe:- Rais Magufuli
Kazi hii tunataka ianze mwaka huu wa fedha, kwa sababu upembuzi yakinifu na usanifu umeshafanyika, kwa hiyo na nyie ongezeni kasi ili mradi huu wote ukamilike, nataka uwe umekamilika kabla sijaondoka madarakani:- Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa Tanzania na nchi nyingine nane zinazotegemea bandari ya Dar es Salaam na kwamba kukamilika kwake kutatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambayo imedharia kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Biashara wa China Mheshimiwa Qian Keming amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kukuza uchumi wa Tanzania, kupiga vita rushwa na kwa namna ya kipekee kwa dhamira yake ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na China na ameahidi kuwa Serikali ya China itaongeza msukumo katika uharakishaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kati.
Mheshimiwa Rais Magufuli nimeielewa dhamira yako na kiu uliyonayo, naona kabisa kwamba dhamira ya kisiasa ipo ya kutosha, tunachotakiwa kukifanya ni kuwasukuma wataalamu wetu waongeze kasi, na mimi nakuahidi kuwa tulikuwa tunakwenda kwa kasi ya kilometa 100 kwa saa, sasa tutaongeza na kwenda kilometa 200 kwa saa:- Waziri Qian Keming.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Dkt. Lu Youqing, Makamu wa Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Sun Ping, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles John Mwijage na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Naibu Waziri wa Biashara kutoka Jamhuri ya Watu wa China Qian Keming aliyefika Ikulu pamoja na ujumbe wake kwa ajili ya mazungumzo Oktoba 14,2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Dkt. Lu youqing aliyefika Ikulu pamoja na ujumbe wa Naibu Waziri wa Biashara kutoka Jamhuri ya Watu wa China Qian Keming.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Makamu wa Rais wa Benki ya EXIM ya China Sun Ping ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Qian Keming kwa ajili ya mazungumzo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Biashara kutoka Jamhuri ya Watu wa China Qian Keming watatu kutoka kulia aliyefika Ikulu pamoja na ujumbe wake kwa ajili ya mazungumzo. Wengine katika picha ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wakwanza (kushoto) Makamu wa Rais wa Benki ya EXIM ya China Sun Ping wapili kutoka (kushoto) Balozi wa China hapa nchini Dkt. Dkt. Lu youqing watatu kutoka (kushoto), Pamoja na Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage wapili kutoka kulia
No comments:
Post a Comment